Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali imefanya Kikao kazi na Wakurugenzi wa Divisheni, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Sheria kutoka Wizara, Taasisi na Halmashauri mbalimbali kilichofanyika tarehe 31 Julai, 2024 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe Balozi Prof. Kennedy Gastorn alianza kwa kuwakaribisha washiriki wote kwenye kikao hicho huku akiwaeleza lengo kuu ni kukumbushana masuala mbalimbali yanayohusu Sheria hususani Miongozo mbalimbali iliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza juu ya suala la uundwaji wa Kamati za Sheria katika ngazi ya Mikoa na Wilaya ambapo alisema, “Napenda kusisitiza kwa kila Mkoa na Wilaya kukamilisha utengenezaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria pamoja na kuwa na mpango mkakati wa namna kamati hizo zitakavyotekeleza majukumu yake, kama ambavyo Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekuwa akisisitiza.”
Vilevile Mhe Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezielekeza Kamati za Mikoa na Wilaya zikae kwa mujibu wa mwongozo wa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili ziweze kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za Wananchi. “Aidha Kamati hizi za Mikoa na Wilaya zifanye Kliniki za Kisheria katika maeneo yao, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipo tayari katika kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati ili waweze kutekeleza majukumu yao”, amesema
Katika hatua nyingine Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewapongeza Viongozi wa Mikoa ya Simiyu, Songwe na Pwani ambao tayari wamekamilisha uundwaji wa Kamati za Ushauri wa Kisheria ” Kipekee nitoe pongezi kwa viongozi wa Mikoa ya Pwani Songwe na Simiyu kwa kufanikisha uundwaji wa kamati za Ushauri wa Kisheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kushiriki katika uzinduzi wa kamati hizo pamoja na Kliniki za Kisheria katika Mikoa hiyo,” ameeleza.
Akimalizia hotuba yake ya ufunguzi Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Balozi Prof. Kennedy Gastorn aliwakaribisha washiriki hao kwenye kikao kazi hicho huku akiwataka kuwa huru na kuuliza pale panapohitaji ufafanuzi wa kina.