Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba na Makubaliano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Sunday Hyera amezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu Divisheni hiyo huku akijikita zaidi kwenye Sehemu za Divisheni, Majukumu pamoja na mwongozo uliotolewa na Divisheni hiyo kuhusu Mikataba
Aidha Bw. Hyera alianza kwa kuzungumzia kuhusu Sehemu (section) zinazounda Divisheni hiyo kuwa ni pamoja na Sehemu ya Mikataba ya Ununuzi wa Umma, Sehemu ya Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa na Sehemu ya Mikataba ya Uwekezaji Maliasili na Fedha. “Sehemu hizo tatu zilizoko kwenye Divisheni ya Mikataba zinaongozwa na Wakurugenzi Wasaidizi,” aliongeza Bw. Hyera.
Akizungumzia majukumu yanayotekelezwa na Divisheni hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba na Makubaliano Bw. Sunday Hyera amesema kuwa jukumu kubwa linalotekelezwa na Divisheni hiyo ya Mikataba ni kufanya Upekuzi wa Mikataba (vetting of contracts). “Ninapoongelea upekuzi wa Mikataba ninamaanisha Mikataba yote ya Ununuzi wa Umma kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2024, ambapo Sheria hii inataka Mikataba yote yenye thamani zaidi ya bilioni moja inapaswa kuletwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya upekuzi.” Alisema Bw. Hyera
Bw. Hyera aliendelea kueleza kuwa Mikataba ya Rasimali za nchi, Uwekezaji na Fedha pamoja na Mikataba yote ya Kimataifa inapaswa kuletwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kufanyiwa upekuzi.
Divisheni hiyo inatoa Ushauri wa Kisheria kwa Serikali na Taasisi zake juu ya namna bora ya uingiaji, utekelezaji na uvunjajii wa Mikataba, Divisheni hiyo pia imekuwa ikitoa Ushauri wa Kisheria kwenye Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayokusudiwa kuridhiwa na Serikali. “Ipo baadhi ya Mikataba ambayo kwa mujibu wa Sheria na tararibu ni lazima Bunge liridhie, hivyo sisi tumekuwa tukitoa ushauri kwenye Mikataba ya aina hiyo kabla ya Bunge kuridhia”. Aliendeleza kueleza Bw. Hyera
Aidha, aliendelea kuelezea namna Divisheni yake inavyoshiriki kwenye majadiliano ya Mikataba ambayo inahusu Serikali na Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa maslahi ya Umma yanazigatiwa, vilevile Divisheni hiyo inafanya utafiti wa Mikataba ya Kitaifa na Kimataifa na imekuwa ikishiriki mikutano mbalimbali ya kikanda na Kimataifa.
Katika hatua nyingine Bw. Hyera alitoa msisitizo kwa Taasisi za Serikali kutumia Muongozo uliotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya Mikataba ujulikano kama “Contract Manual” ambapo Bw. Hyera alisema “Contract Manual ni muhimu sana kwa Taasisi za Umma kwakuwa inatoa Mwongozo wa namna ya uingiaji, upekuaji, utekelezaji na uvunjaji wa Mikataba mbalimbali, hivyo wanasheria walioko kwenye Taasisi za Umma wanapaswa kuifuata Manual hii katika utekelezaji wa Mikataba”.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Divisheni ya Mikataba na Makubaliano alimalizia kwa kuzitaka Taasisi mbalimbali kuzingatia taratibu na Sheria wakati wa uingiaji wa Mikataba, huku akieleza kuwa milango ya Ofisi hiyo iko wazi kwa Taasisi kuja kufuata Ushauri wa Kisheria kuhusiana na mikataba. ” Niziombe Taasisi za Umma kuwashirikisha Wanasheria walioko kwenye maeneo yao katika hatua zote za uingiaji wa Mikataba ambayo Taasisi hizo imepanga kuingia” alimalizia Bw. Hyera