Wananchi Mkoani Mbeya wametakiwa kuacha kuchukua mikopo inayoumiza maarufu kausha damu, badala yake kuchukua mikopo kwenye taasisi rasmi za kifedha ambazo ziko kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumza wakati hafla ya ufunguzi wa tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar(PBZ) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Dkt Tulia Ackson, amesema watu wengi wameumizwa na mikopo ya kitapeli kwenye mitandao na mitaani hivyo ni wakati wa kubadikika na kuchukua mikopo kupitia Benki ya PBZ.
Mhe.Dkt.Tulia ameipongeza benki ya PBZ kufungua tawi ambalo litaongeza kasi ya maendeleo Nyanda za Juu Kusini kwa vile wafanyabiashara,wajasiriamali, watumishi na wakulima wataitumia katika kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya PBZ Bw. Arafat Haji amesema kufunguliwa kwa tawi la benki hiyo ukanda huu Nyanda za Juu Kusini hasa Mkoa wa Mbeya kutawafanya wafanyabiashara wa zao pendwa la mchele wa Mbeya kutoka Zanzibar kuwa salama kwa fedha zao kupitia tawi lililofunguliwa eneo la Mafiati jijini Mbeya.
Bw. Haji ameeleza kuwa benki hiyo iliyoanzishwa tarehe 30 Juni, 1966 kwa majibu wa sheria za makampuni kifungu cha 153 inamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia mia moja(100%) na inashika nafasi ya saba kwa ukubwa wa mabenki ikiwa na rasilimali ya Trilioni mbili nukta mbili(Tril2.2).
Benki ya PBZ imefungua matawi kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara na Mbeya, hivi karibuni itafungua matawi mengine Mwanza, Arusha na Tanga, mpango ukiwa ni kuifikia mikoa yote nchini.