Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha akizungumza katika kongamano la wafugaji Tanzania lililofanyika wilayani Igunga mkoani Tabora
Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mrida Mshota akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani mbele ya wafugaji .
Mmiliki wa Kiwanda cha kuchakata maziwa cha Kahama Fresh kutoka mkoani Kagera Jossam Ntageki, ambaye ameomba kupewa eneo mkoani Tabora kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata nyama.
Viongozi wa Chama Cha Waganga wa Tiba asiliana na wazee wa kimila wakifuatilia kongamano la Chama Cha Wafugaji Tanzania
Baadhi wafugaji zaidi 3000 wakifuatilia kongamano
……………
CHAMA Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimemchangia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kiasi cha shilingi milioni Moja kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuwania Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi ujao wa 2025.
Akizungumza katika kongamano hilo Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mrida Mshota alisema wanachama wa Chama wameamua kutoa mchango huo ili kuunga juhudi za Rais katika kongamano hilo lililofanyika kwenye kiwanja cha kumbukumbu ya Sokoine Wilayani Igunga Mkoani Tabora na kuhudhuriwa na zaidi ya wafugaji 3000 kutoka Kanda Nane (8) hapa nchini
Alisema kuwa, wametoa fedha hizo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia za kuleta Maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatambua wafugaji jambo ambalo limechochea kukuwa kwa Sekta ya ufugaji na kuongeza wawekezaji katika sekta ya hiyo.
“Toka tumeingia madarakani mimi na wenzangu tulikuta migogoro na changamoto nyingi sana, niwaambie ndugu zangu wafugaji kwa miaka hii mitatu Rais Dkt. Samia alipoingia madarakani bajeti ya Wizara ya Mifugo na Kilimo ilikuwa bilioni 166 lakini mwaka huu wabunge wamepitisha bilioni 460 sasa muone kwamba serikali ilivyofanya kazi kubwa, kwa hiyo wafugaji tusikae kama mabubu hivyo tuseme mambo ambayo Rais ametufanyia kwa maendeleo yetu, ” alisema Mshota.
” Mimi sina biashara zaidi ya ufugaji wa ng’ombe, kwa hiyo ndugu zangu wakasema Mwenyekiti mwaka kesho ni mwaka wa uchaguzi sisi wafugaji tunakwendaje, mimi nikawaambia twendeni na Samia kazi kubwa imefanyika, ndugu mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa peleka salamu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwambie tunamuunga mkono na tunampa miaka mingine mitano tena na leo tunatoa sh. milioni moja ya kumchukulia fomu na tutaendelea kuchanga zaidi kufanikisha anashinda kwa asilimia 96.6 kwa hali na mali, ” alisema Mshota.
Naye Mlezi wa Chama hicho Taifa Joseph Makongolo alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imetatua matatizo ya wafugaji kwa kiwango kikubwa hivyo amemuomba Rais Dkt. Samia kuongeze maeneo kwa wafugaji na mabwawa yanayochimbwa kwa ajili ya maji kuwekwe mabirika ya kunyweshea ng’ombe.
“Nina toa nasaha kwa wafugaji wenzangu kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu jambo hili litamrahisishia Mhe. Rais na viongozi wake kufanya kazi kwenye suala letu la ufugaji na kupata ufugaji wenye tija, pia ninaomba kwetu wafugaji kusitisha migogoro na wakulima kwani sisi sote ni watoto wa baba na mama moja, kwa asilimia fulani sisi ndio tumekuwa chanzo cha migogoro ya mipaka ambayo imezuiwa naomba tuache migogoro kwanye maeneo yasiyo yetu, ” alisema Makongolo.
Huku mmoja wa wafugaji na mmiliki wa kiwanda cha kuchakata maziwa ya ng’ombe cha Kahama Fresh Jossam Ntengeki alisema kuwa ameamua kuwekeza nchini kutokana na kuisha kwa migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo hivyo amaanzisha kiwanda cha kuchakata maziwa mkoani Kagera na sasa anaangalia namna ya kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama hapa nchini katika mkoa wa Tabora hasa wilayani Igunga na baadaye atajenga kiwanda cha kuchakata ngozi.
Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha akizungumza katika kongamano hilo alisema kuwa amepokea maoni ya wafugaji nchi nzima kupitia kongamano hilo na amepokea fedha hizo na atampelekea Rais Dkt Samia ikiwa ni pamoja na kufikisha salamu zao za kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.
Aidha aliwapongeza viongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora kwa kuhakikisha mkoa umekuwa shwari.
“Ni wahakikishieni wafugaji Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anawapenda sana, mengi mmesema wenyewe na mmeona mnaye muhitaji ni Dkt. Samia awe Rais wa nchini hii ujumbe wenu ntaufikisha kwa Rais amenileta Tabora niwalinde nyinyi na ndio maana nimekuja na RPC Richard Abwao na OCD wa Igunga Meshaki Sumuni hawa ndio viongozi wetu wa Jeshi la Polisi mkoani kwetu ninawaomba kuwalinda wafugaji na kuwakamata watu wote wale wanaowatapeli, ” alisema Chacha.
Alimaliza kwa kusema kuwa, kila litakapo jengwa bwawa la maji zitajengwa sehemu za kunyweshea ng’ombe na kila eneo litakapo pita bomba la maji kutoka Ziwa Victoria wataweka sehemu za kunyweshea, pia amewataka wafugaji kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ikiwa ni pamoja na kuandikisha watoto shuleni.
Hata hivyo alitumia nafasi hioyo kumtaka mwekezaji Jossam Ntengeki na wengine kuwekeza mkoani Tabora kwani maeneo ya uwekezaji ni mengi.