Na Sophia Kingimali.
NAIBU Spika la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 19 ya Chuo Cha Ufundi Stadi cha Furahika ambacho kipo Buguruni Malapa jijini DAR ES Salaam ambapo mahafali hayo yatafanyika Agosti 3,2024 huku wahitimu 120 wa kozi mbalimbali ikiwemo Ualimu, Sekretari, Hotel na nyinginezo ambazo zipo chini ya Veta na mhitimu ambaye amefanya vizuri kwa kila kozi atapewa zawadi.
Haya yamebainishwa leo na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt David Msuya leo Julai 29, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema wazazi na walezi wa vijana hao wanahitimu na wengineo wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo muhimu katika maisha ya watoto wao.
“Tunayofuraha kubwa kwenda kusheherekea mahafari ya 19 tangu chuo hiki kianzishwe na mgeni wetu ataakuwa Mbunge wa Ilala, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, hivyo tunawaomba wazazi ama walezi wa vijana ambao wanahitimu mafunzo haya waje kwa wingi kufurahia kwa pamoja na watoto kwa siku hii muhimu kwa maisha yao.
“Pia mahafali haya yanafungua milango kwa kundi lingine kujiunga na muhula mpya wa masomo kwa miezi sita na mwaka mmoja kwa kozi ya hoteli, Bandari na nyinginezo na tunawaomba vijana ambao wameishia darasa la saba, kidato cha pili ama kidato cha nne na wakashindwa kupata alama nzuri za kuendelea na masomo waje hapa kutimiza ndoto zao katika elimu,” amesema
Ameongeza kuwa muhula mpya unatarajia kuanza Septemba 10 mwaka huu pamoja na kozi mpya ya Uhariri na upigaji picha za video (Video Production) itaanza kufundishwa chuoni hapo jambo linalotanua wigo wa vijana wengi kutimiza ndoto zao kwa kupata ujuzi wa kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.
Amesisitiza kuwa yote yanafanyika kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kufungua milango ya uwekezaji na kusababisha mashirika mengi kuja kusaidia vijana na wao kutoa elimu bure na jambo linalitakiwa sasa ni vijana kutumia fursa hiyo vizuri ili kujikomboa katika dimbwi la umasikini.
Dkt Msuya ameongeza kuwa wanafunzi ambao wanajiunga na chuo hicho wanapata fursa ya kutafutiwa sehemu ya mafunzo kwa vitendo na wale wanaofanya vizuri wanajiweka katika mazingira mazuri ya kupata ajira baada ya kumalizi masomo yao
Sambamba na hayo Dkt Msuya ametoa rai kwa wadau mbalimbali kujitokeza chuoni hapo kwa kuwapa msaada wa vitendea kazi ikiwemo komputa.
“Niwaombe wadau wa ndani kusapoti juhudi hizi zinazofanywa na rais pamoja na washirika wa maendeleo kutoka nje ambao ndio wanatusaidia hapa chuoni tuna uhaba wa komputa kwa ajili ya kufundishia watoto wetu na ukiangalia sasa hivi duniani ipo katika ulimwengu wa Teknolojia hivyo tunawaomba wadau wajitokeze kutusaidia”,Amesema Msuya.