Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
SERIKALI imekiagiza Chama cha Netbali Nchini CHANETA, kukaa na Baraza la michezo Nchini BMT, ili kujadili changamoto zilizopo zinazokwamisha maendeleo ya mchezo huo ili izifanyie kazi Ili waweze kuwa na mvuto kama miaka iliyopita.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Hamisi Mwinyijuma, maarufu Mwana F.A.alipokuwa akifungua Mkutano mkuu wa mwaka wa Chaneta, kwenye Ukumbi wa mikutano ya Kimataifa, AICC, Jijini Arusha.
Amesema Serikali imepanga asilimia 25% kudhamini kila mchezo hivyo akaitaka Chaneta wamalize migogoro ya ndani na Serikali itatoa ufadhili wa mchezo huo sanjari na kufanya jitihada za kurejesha wadhamini.
Amesema mchezo huo ambao miaka iliyopita ulikuwa namba mbili Nchini kwa kupendwa umepoteza umaarufu na mvuto kwa kuwa imejaa migogoro hivyo inakuwa sio rahisi kupata Wadhamini kwa kuwa mchezo huo umegalagazwa na kupakwa matope.
Kuhusu kuleta wataalamu wa mchezo huo ili kuwanoa wataalamu waliopo au kuwapeleka nje wataalamu hao, Waziri Mwinyijuma, amesema Serikali italifanyia kazi lengo ni kupata wataalamu mbalimbali wakiwemo makocha na waamuzi ili kuendeleza mchezo huo nchini.
Amesema kuanzia sasa Viwanja vyote vya michezo vinavyojengwa lazima viwe na eneo la kucheza Netbali ili kuendeleza na kuufufua mchezo huo ambao umeporomoka na kupoteza mvuto
Amesisitiza uchaguzi wa timu ya taifa usiwe wa upendeleo ,yafanyike maandalizi ya kutosha ambayo yanawezesha timu ya taifa ifanye vizuri vinginevyo Serikali haitota ruhusa kushiriki michezo hiyo.
Amesema mambo yanayokwaza Serikali ni maendeleo hafifu ya timu ya taifa ya Netbali na maandalizi yake mchezo huo ni miongoni mwa michezo inayopewa kipaumbele lakini inaikwanza Serikali.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Netbali taifa CHANETA, Dkt Devotha Marwa, amesema kuwa lengo la mkutano mkuu huo ni kujadili maendeleo ya mchezo wa Netbali nchini. kupitia Katiba ya Chaneta,na kupokea Taarifa ya fedha .
Amesema changamoto iliyopo ni Chaneta kukosa wadhamini wakudumu hivyo kuathiri maendeleo ya mchezo huo .
Ameziomba Serikali kuleta wataalamu wa michezo wa Netbali ili waje kuendeleza mchezo huo au Serikali igharimie wataalamu waliopo kusoma nje Ili warejee kuendeleza mchezo huo Nchini .
Mmoja wa wadhamini wa Mkutano huo, Meneja wa Kanda ya Kaskazini kutoka Benki ya NMB, Baraka Ladislaus amesema kuwa wamesapoti mkutano huo kiasi cha Shilingi milioni nane ili kuwasaidia kufanikisha malengo waliojiwekea yatimie.
“Tumefanya hivi kwa kutambua umuhimu wa michezo kwenye jamii lakini pia kundi kubwa la wanamichezo ambao ni wateja wetu hivyo tutaendelea kuunga mkono jitihada za michezo nchini kumsaidia Rais wetu kuhakikisha wanafanikiwa kwenda kimataifa na kuitangaza nchi yetu vema” amesema Baraka.
Amesema, kufanya hivyo ni kuzidi kuisogeza Taasisi hiyo karibu na wananchi kujua changamoto zao lakini pia kubuni bidhaa mbalimbali zenye kuleta masuluhisho ya kifedha.
“Kwa sasa tunaendelea kutoa elimu jumuishi ya kifedha na kufungulia wateja akaunti mpya ya NMB pesa kwa shilingi 1000 na inawasaidia kupata hadi mikopo ya mshiko fasta bila kudai makabrasha yoyote” amesema.









