NA Neema Mtuka
RUKWA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo Mkoani Rukwa Shafi Mpenda ameitaka idara ya afya wilayani humo kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa ujenzi wa vyoo bora ili kuepukana na milipuko ya magonjwa ikiwemo kipundupindu.
Mpenda ameyasema hayo baada ya kukutana na timu ya uhamasishaji wa kampeni ya mtu ni afya kutoka wizara ya afya ofisini kwake na kubainisha kuwa lengo la serikali ni kuiwezesha jamii kuwa na vyoo bora kutoka asilimia 74 mwaka 2023 na kufikia asilimia 100 ifikapo 2023.
Aidha Mpenda amesisitiza kuwa ni muhimu idara ya afya wilayani humo ikaendelea kuihamasisha jamii kuboresha usafi wa mazingira katika makazi yao biashara na maeneo ya umma.
Licha ya hilo amesisitiza jamii kubadili tabia kuhusu ulaji unao faa na mtindo wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi ya mwili kwa njia ya michezo ili kuboresha afya,kwa kuwa na utaratibu endelevu wa kufanya mazoezi ya mwili.
Afisa afya mkoani humo Martine Emmanuel amesema jamii inawajibu wa kupambana na kila aina ya unyanyapaa dhidi ya wanawake au wasichana walio katika hedhi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na aina za unyanya paa na mila zilizopitwa na wakati.
Amesema kuwa ni wakati wa kufanya kweli na kuachana na mila potofu zilizopitwa na wakati na badala yake jamii inapaswa kuwalinda watoto wa kike kila wakati kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwemo taulo za kike.
‘’Kupitia kampeni hii tutahamasisha na kusimamia jamii kuwa na mazingira safi na salama ikiwemo kuondosha na kusimamia jamii kuwa na mazingira safi na salama’’ alisema Emanuel.
Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Matai wilayani Kalambo akiwemo Sospeter Michese amesema hapo zamani walikuwa wanajisaidia vichakani hali ambayo iliwasababishia milipuko ya magonjwa lakini kwa sasa kupitia elimu waliyopewa wataondokana na changamoto hiyo.
Kampeni hii inafanyika tena baada ya miaka 50 kutokana na umuhimu wake katika kulinda na kuboresha afya.
Katika miaka 5 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza 1973-1978 kampeni ilisaidia kuongeza kaya zenye vyoo nchini kutoka 20% hadi 78%
Pia ilisaidia sana kuboresha hali ya lishe bora nchini kutokana na manufaa hayo serikali ya awamu ya 6 inaendeleza mafanikio hayo.
Kampeni hii inafanyika nchi nzima na timu ya uhamasishaji ikiongozwa na Mrisho Mpoto (MJOMBA ) imeanza kazi mkoani Rukwa kwa lengo la kuendeleza ustawi bora wa afya za wananchi.
Kampeni hii imebeba kauli mbiu inayosema FANYA KWELI ,USIBAKI NYUMA MTU NI AFYA .