Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imejipanga kuhakikisha ifikapo Desemba 2024 vijiji vyote 519 Mkoani Kilimanjaro viwe vimeunganishwa na umeme.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amebainisha hayo mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa Julai 29 Mkoani Kilimanjaro wakati wa utambulisho wa Wakandarasi walioshinda zabuni ya kusambaza umeme katika vijiji 13 vilivyokuwa vimesalia.
“Hadi sasa tumeunganisha umeme katika vijiji 506 kati ya vijiji 519 ambayo ni sawa na asilimia 97.49 Mkoani hapa; na leo hii tupo hapa kutambulisha Wakandarasi watakaotekeleza miradi katika vijiji hivi vilivyosalia na vitongoji 34,” amebainisha Mhandisi Olotu.
Mhandisi Olotu amebainisha kuwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro; REA inatekeleza jumla ya miradi mikubwa mitatu.
“Mradi wa shilingi bilioni 13.1 wa kusambaza umeme vijijini, mradi wa bilioni 8.8 wa kusambaza umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa bilioni 1.7 wa kusambaza umeme katika vituo vya afya na visima vya maji,” amesema Mhandisi Olotu.