Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amezindua tamasha kubwa la utalii ndani ya Wilaya ya Kisarawe liitwalo “Bata Msituni Festival,” litakalofanyika kwa siku tatu mfululizo.
Tamasha hilo linalotarajiwa kuanza Septemba 6 hadi 8 , 2024, linatarajiwa kukuza sekta ya utalii katika Wilaya ya Kisarawe kupitia Hifadhi ya Mazingira ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, iliyoko kilometa 6 kutoka Gongolambo na kilometa 26 kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mheshimiwa Magoti alisisitiza umuhimu wa tamasha hili katika kukuza utalii na urithi wa kitamaduni wa Kisarawe huku akisisitiza umuhimu wa kulinda misitu asili inayochangia uzuri wa eneo hilo.
“Tamasha hili ni kubwa, litashirikisha nchi tatu kutoka Afrika Mashariki na litapambwa na shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maonyesho ya sanaa za kitamaduni, maonyesho ya bidhaa za mikono, na muziki mzuri kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi.
Kisarawe tumejipanga kuwapa wageni burudani ya kipekee kuanzia ngoma za utamaduni, nyama pori, michezo ya kuvua samaki, kutembea msituni, riadha, baiskeli na pikipiki. Kifupi, tamasha hili si la kukosa,” alisisitiza.
Magoti aliongeza kuwa tamasha hilo pia linalenga kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya utalii nchini, na aliwataka wadau kujitolea kudhamini.
Baraka Mtewa, Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Kisarawe, alisema TFS imejipanga kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaofika katika hifadhi hiyo wanapata huduma na uzoefu wa kipekee huku akiwahakikishia usalama na malazi ya kutosha.
Innocent Kabaitilaki, Mratibu wa Tamasha la Bata Msituni, alisema chaguo la Hifadhi ya Msitu wa Pugu kama sehemu ya tamasha linaonyesha dhamira ya tukio hilo kuangazia uzuri wa asili wa Tanzania na kukuza utalii endelevu.
“Tamasha la mwaka huu limevutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi, natutakuwa na matukio ya awali Septemba 3 hadi 6! Niwasihi wananchi kukata tiketi mapema kupitia tovuti rasmi ya Tamasha la Bata Msituni, www.batamsitunifestival.com, au kupitia programu ya tukiio,” alisema Kabaitilaki.