Na Mwandishi Wetu- Zimbabwe
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubaliana kushirikiana na Chuo cha Mafunzo ya Mapishi cha Basque (Basque Culinary Center) cha nchini Uhispania kilichojikita katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti, ubunifu na kufanya uendelezaji wa utalii wa vyakula (Gastronimy Tourism) na lishe.
Lengo la kushirikiana na chuo hicho kinachoongoza duniani kwa Sayansi ya Utalii wa Vyakula, Utafiti na Ubunifu ni kukuza Utalii wa Vyakula nchini Tanzania.
Hayo yamebainika leo Julai 28, 2024 katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Mafunzo cha Basque, Joxe Mari Aizega wakati wa ziara ya kutembelea Kijiji cha Utamaduni cha Umuzi kilichopo jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism).
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki ameomba mashirikiano na chuo hicho katika utoaji wa elimu ya mapishi, kuwajengea uwezo wapishi wa nchini Tanzania pamoja na wakufunzi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, pia kuendeleza tafiti za vyakula, maendeleo ya utalii wa mapishi na namna ya kuboresha vifaa vya mapishi.
Aidha, Mhe. Kairuki ameomba mashirikiano katika ukuzaji wa mitaala ya mapishi kwa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) , shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo binafsi nchini vinavyojishughulisha na taaluma za mapishi ili kuikuza kada hiyo.
Katika hatua nyingine , Waziri Kairuki amekiomba chuo hicho kushirikiana na Tanzania katika kuandaa programu mbalimbali za mafunzo kwa wapishi wa nchini Tanzania na kuona namna ya kuwaelimisha jinsi ya kujitangaza na kuwapa nyenzo za kutafuta masoko ili waweze kuuza huduma zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Mapishi cha Basque, Joxe Mari Aizega amesema taasisi yake iko tayari kushirikiana na nchi zinazotaka kuendeleza Utalii wa Vyakula na pia kuhakikisha ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Tanzania unakuwa thabiti na wa muda mrefu.
“Tumejitolea na tunashirikiana na nchi ambazo zina mikakati thabiti katika Utalii wa vyakula kwa sababu lengo la taasisi yetu ni kukuza utalii wa utamaduni” amesema.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey, Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri, Jesca William na Afisa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Matatizo Kastamu.