Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa,akizungumza na abaadhi ya wananchi waliofika katika kituo cha afya Mtakanini kupata kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa za uchunguzi wa magonjwa ya sukari,saratani ya matiti na mlango wa kizazi na tezi dume kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Taifa MUhimbili wakiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu Profesa Mohamed Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohmaed Janabi katikati,akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa wa kushoto,Diwani kata ya Msindo Lemna Nchimbi kushoto,Mganga Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Aroun Hyera aliyevaa kaunta suti na Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Mtakanini Dkt John Chacha pamoja na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wanaotoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa magonjwa ya Saratani ya mlango wa uzazi na matiti,tezi dume na sukari katika kituo cha afya Mtakanini
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi,akizungumza na wanachi waliofika kwenye kambi maalum ya matibabu ya magonjwa ya Saratani ya matiti,mlango wa uzazi,tezi dume na sukari iliyopo katika kituo cha afya Mtakanini kata ya Msindo wilayani Namtumbo.
…………….
Namtumbo
Profesa Janabi,ameungana na timu ya Madaktari Bingwa watatu wanaotoa huduma za uchunguzi na matibabu kwa magonjwa ya saratani ya mlango wa kizazi,matiti na sukari kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Namtumbo na wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma za matibabu katika kituo hicho,Profesa Janabi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma zinazotolewa bure ili waweze kufahamu hali ya afya zao na kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Profesa Janabi ni kwamba,kambi hiyo ni muhimu sana kwani hivi sasa idadi ya watu wanaofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kupata huduma ya kusafisha figo ni kati ya 120 hadi 130 kila siku.
Alisema,sababu kubwa inachangiwa na mtindo wa maisha,hivyo jamii inatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuepuka kula vyakula vinavyoweza kupelekea watu kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo Kisukari na figo ambayo husababishwa na lishe.
Alisema,kasi ya ongezeko la wagonjwa wa figo inaonesha watu wana mtindo wa maisha usiofaa ikiwemo ulaji mbaya wa vyakula,matumizi makubwa ya pombe na wakati mwingine kutumia Dawa za kutuliza maumivu bila kupata ushauri wa Daktari.
Alieleza kuwa,kwa kawaida mwili hubadilisha sukari na wanga na kuwa mafuta,hivyo ni muhimu kupunguza matumizi ya vitu hivyo kwani kinga ni bora kuliko tiba na kusisitiza kuwa ni vyema kupunguza matumizi ya sukari na kufanya mazoezi mara kwa mara.
Alisema,watu wenye uzito mkubwa kama mwanaume anavaa suruali kiuno zaidi ya sentimeta 40 na wanawake sentimeta 35 na kuendelea basi wanapaswa kuchukua hatua za haraka kupunguza miili yao kabla hawajaingia kwenye hatari ya kupata magonjwa yasioambukiza.
Kwa upande wake kiongozi wa Timu ya Madaktari hao kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt Joackim Anjelo alisema,kwa muda wa siku tatu wamehudumia jumla ya wagonjwa 232,wanawake 184 na wanaume 76 wenye matatizo mbalimbali.
Alisema,kwa upande wa magonjwa ya ndani ikiwemo sukari,presha na moyo,homoni na vidonda vya tumbo, wagonjwa 102 wamepatiwa huduma na kati ya hao 42 wanasumbuliwa na tatizo presha.
Akizungumzia magonjwa ya mfumo wa mkojo na uzazi kwa wanaume pamoja na upasuaji alisema,wamehudumia jumla ya wagonjwa 64 ambapo 32 wamekutwa na tatizo la tezi dume na wengine wana matatizo ya ugumba,upungufu wa nguvu za kiume,ngili,saratani ya kibofu cha mkojo na mirija ya mkojo kuotea nje ya mfumo.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha huduma za matibabu zinazofahamika kwa jina la Dkt Samia Suluhu Hassan Mkoba ambazo zimewafikia watu wengi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini.
Alisema,kwenye vijiji kuna watu wengi wenye matatizo mbalimbali ya afya,lakini wanashindwa kupata matibabu kutokana na changamoto ya kufikiwa huduma za uchunguzi na matibabu za kibingwa kuishia kwenye Hosptali za mikoa.
Kawawa,ameiomba serikali kuona umuhimu wa kuajiri Madaktari Bingwa wengi zaidi wataokwenda kufanya kazi kwenye vituo vya afya ambavyo vingi vinapatikana vijijini ili waweze kutoa huduma kwa wananchi wanaopatikana vijijini na ndiyo nguvu kazi kubwa ya Taifa.