NAIBU Waziri wa Maji,Mhandisi Kundo Matthew,amekerwa na vitendo vya wizi wa dira za maji na kuisababishia serikali hasara,huku akiwataka wananchi wa Wilaya ya Ilemela na Jiji la Mwanza,kujiepusha navyo.
Pia amewataka wananchi wawe walinzi wa miundombinu ya miradi ya maji na kulipa Ankara za matumizi kwa wakati,miradi iwanufaishe na kuwa endelevu.
Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo leo,alipozungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu katika mkutano wa hadhara uliolenga kusikiliza na kutatua changamoto na kero za maji zinazowakabili wa wananchi wa Ilemela na Jiji la Mwanza.
Amesema rasilimali ya maji ni uhai,inazalishwa kwa gharama kubwa,hivyo wananchi wasikwepe kulipa badala yake wadhibiti matumizi watumie kulingana na uwezo wa kipato.
“Msidanganyike kutoa fedha (rushwa) kuficha madeni kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu,deni lako halisi haliwezi kufutwa katika mfumo tusikwepe,tukatumie kulingana na kipato,tukifanya hivyo malalamiko ya kubambikizwa Ankara yatapungua,”amesema Naibu Waziri huyo wa Maji.
Amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha za miradi ya sekta ya maji,lakini tatizo la uhaba wa maji jijini Mwanza,chanzo chake hakitoshelezi,mradi wa Igombe-Kabangaja ukikamilika utaondoa changamoto hiyo kwa kutoa maji ya uhakika.
“Niwashukuru kwa kuwa wakweli na serikali haitawangusha,nchi hii hatutaijenga kwa kudanganyana na ukweli utatusaidia kujenga badala ya kubomoa,uchungu na hisia zenu hatutazipuuza tutaendelea kuzifanyia kazi kwa kuongeza mtandao wa maji licha ya changamoto ya bajeti,”amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (NWAUWASA),Neli Msuya amesema mradi wa Matokeo ya Haraka unaogharimu sh.bilioni 4.7 umechelewa kukamilika sababu ya ukosefu wa fedha.
“Sh.milioni 500 zilitolewa kuboresha mfumo wa maji Buswelu,kutokana na ukubwa wa tatizo fedha hizo hazikukidhi kufikisha maji maeneo yote,tulibuni Mradi wa Matokeo ya Haraka wenye thamani ya sh.bilioni 4.7,tumepokea sh.bilioni 1.7 tukalaza mabomba kilometa 14,”amesema.
Naye Mbunge wa Ilemela (CCM),Dkt.Angeline Mabula amesema juhudi za Rais Dk.Samia kumtua mama ndoo kichwani zimeanza kuonekana ambapo Ilemela imepata mradi wa Maji wa Igombe-Kabangaja wenye thamani ya sh.milioni 800 ukikamilika pamoja na chanzo cha Butimba,maji yatatosheleza.
“Tunaishukuru serikali kwa Mradi wa Matokeo ya Haraka,umekuwa na tija kwa kupunguza kero ya maji,changamoto ni vifaa na naamini itatatuliwa,niombe Mkurugenzi wa MWAUWASA mifumo ikifunguka fedha zikaanza aje hapa Buswelu kuondoa tatizo la maji,”amesema.