Na Mwandishi Wetu
Mgombea wa Urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Emmanuel Muga, amekanusha madai ya kuwepo kwa uonevu katika uchaguzi wa Urais ndani ya chama hicho. Muga alisisitiza kuwa uchaguzi huo unaendeshwa kwa haki, tofauti na madai yanayotolewa na baadhi ya watu.
Muga alitoa kauli hiyo katika mdahalo wa wagombea ulioendeshwa na kituo cha televisheni cha Star TV, ambapo wagombea wote sita walishiriki. Alikuwa akijibu swali lililoulizwa na mwananchi kuhusu kuenguliwa kwa mgombea mwenzake, Boniface Mwabukusi, na kisha kurejeshwa tena kwa amri ya mahakama.
“Si vyema kuhusisha siasa katika uchaguzi huu na kukuza mambo ambayo hayapo kwenye mchakato wake. Uchaguzi unaendeshwa kwa haki, tofauti na inavyotaka kuaminishwa kwenye jamii,” alisema Muga.
Muga aliongeza kuwa kamati zilizoundwa kusimamia uchaguzi huo ni za kitaaluma na zinaendeshwa na mawakili wenyewe. “Hakuna mtu mwingine kutoka nje. Sisi wanasheria tunakutana mara nyingi na maamuzi kama haya, na ni vema tuelewe mfumo wa utoaji haki uliopo,” alisisitiza Muga.
“Kwa kamati ya uchaguzi ya TLS, Mwabukusi alipata haki na kuruhusiwa kugombea, lakini kamati ya rufani ambayo inaundwa na mawakili ikamwengua. Hata hivyo, Mahakama Kuu ikamrudisha. Huu ni mfumo ambao tumeuzoelea sisi, lakini nje umeelezwa vibaya, utafikiri sisi si wanasheria. Tusikuze jambo,” alisema Muga.
Mbali na Muga, wagombea wengine wa nafasi hiyo ya Urais wa TLS ni Sweetbert Nkuba, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, Kapteni Ibrahimu Bendera, na Boniface Mwabukusi.