Na Ashrack Miraji (Fullshagwe) Same Kilimanjaro
Katibu Tawala Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro,Upendo Wella amewataka wananchi kuzingatia ulaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi lishe vitakavyosaidia kuboresha afya zao.
Wella ameyasema hayo wakati akimuakilisha Mgeni rasmi,Mkuu wa Wilaya ya Same,Kaslida Mgeni kwenye kikao cha matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kwa wadau wa lishe wilayani hapo.
Amewataka wadau wa lishe kushirikiana kwa pamoja na watendaji kata na mdiwani kuitoa elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka ili wajue umuhimu na faida za kiafya kupitia kula vyakula vyenye virutubishi.
“Jitihada ya serikali katika kupunguza matatizo ya lishe duni yanatokana na upungufu wa virutubishi muhimu ambayo ni madini ya chuma, madini ya joto na vitamin A. Hivyo niwaombe vongozi wote wa kata,viongozi madiwani ambao mmepata elimu hii,basi mkawahamasishe wananchi kwa maslahi mapana ya taifa letu” amesema.
Katibu huyo amesisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kupunguza matatizo ya lishe duni kama vifo vya mama wajawazito pamoja na watoto wachanga,matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa watoto kutokana na matatizo yanayohusianana na upungufu wa damu mwilini.
“Hivyo niwaombe viongozi wa ngazi ya serikali za Mitaa pamoja na idara inayohusika na lishe kwenda kuwapa Elimu Wananchi”.
Kwa upande wake,Afisa Lishe Mkoa wa Kilimanjaro,Rehema Napegwa alieleza juu ya takwimu za udumavu wa watoto kuwa zimepungua kitaifa, ambapo zinaonyesha hivi karibuni mwaka 2022 kuwa imepunguwa kutoka asilimia kubwa hadi kufikia sasa asilimia 30% na kwa mkoa wa Kilimanjaro ni asilimia 20% ya tatizo la Udumavu.