Na Dk. Reubeni Lumbagala
Kwa mujibu wa falsafa ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ili nchi iweze kupata maendeleo ya kweli inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Kwamba uwepo wa mambo haya manne na yakatumika kikamilifu kunaweka uhakika wa jamii na nchi kwa ujumla kupata maendeleo ambayo ndiyo kiu kubwa ya kila mwananchi. Wananchi wanataka maendeleo na ustawi bora ili kufurahia zawadi ya maisha hapa duniani. Ndiyo maana wananchi wanajituma kila siku katika shughuli za uzalishajimali ili kupata vipato vitakavyowawezesha kukidhi mahitaji yao na kupiga hatua za kimandeleo.
Tukirudi katika mambo manne aliyoyasema Hayati Baba wa Taifa ili nchi iweze kupata maendeleo, kwa leo nataka nizungumzie eneo moja la uongozi bora kama chachu ya kufikia maendeleo. Uongozi bora ni kuongoza kwa kufuata kanuni na sheria kwa manufaa ya wale wanaoongozwa. Uongozi bora ni ule wenye kuzingatia mahitaji ya watu, kujituma, kupigania haki kwa kuhakisha maslahi ya wengi yanazingatiwa. Aidha ni uongozi unaosikiliza hoja za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi. Uongozi bora hauna ubinafsi wala umimi, bali unasimama na mahitaji ya wananchi.
Maendeleo ya kweli katika jamii na nchi kwa ujumla yatapatikana endapo wananchi watachagua viongozi bora ambao watasimama na kupigania haki na mahitaji ya wananchi na si mahitaji binafsi ya kupata umaarufu na kujilimbikizia mali. Mwishoni mwa mwaka huu, nchi yetu inatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu. Uchaguzi ni njia ya kidemokrasia ya wananchi kuchagua viongozi bora watakaowatumika na kuwa daraja la kufikia maendeleo. Uchaguzi ni fursa kwa wananchi kusema nani wana imani naye na kuamini kuwa anaweza kukidhi matarajio yao na kujenga jamii na nchi yenye amani na maendeleo.
Ndiyo maana ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwa kusikiliza sera za wagombea ili kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi ndani ya mchakato wa ndani wa vyama vya siasa na mwisho katika uchaguzi wa jumla unaohusisha wagombea kutoka vyama vyingine katika eneo husika. Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwalalamikia viongozi wao, lakini cha ajabu baadhi ya wananchi hao wanaolalamika ndiyo hao hao ambao hawakushiriki kupiga kura na hivyo wanaongozwa na viongozi waliochaguliwa na watu wengine! Hivyo basi, njia nzuri ya kupata viongozi bora ni wananchi wenyewe kushiriki kuwasikiliza wagombea na mwisho kufanya maamuzi sahihi ya kuchangua viongozi kwa vigezo madhubuti vya kupata viongozi bora na si kwa mazoea au kuhongwa na wagombea.
Mwanamajumui wa Kenya, Profesa Patrick Loch Lumumba alipata kusema kwamba wakati wa uchaguzi ni sawa na mtu kupewa hundi (blank cheque) ili aandike mwenyewe anachotaka. Kwa hiyo vyama vinapopitisha mgombea mbovu na hatimaye wananchi kumchagua wanakuwa wametumia vibaya hundi hiyo muhimu. Profesa pia huwa anawaashangaa Waafrika kuchagua viongozi wabovu na kisha kulalamika akisema ni sawa na kununua pikipiki na kutarajia ifanye kazi kama benzi! Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala kina kiu ya kutaka kuendelea kuwatumikia wananchi katika kipindi kingine cha miaka mitano katika chaguzi zote yaani uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu na ule mkuu wa mwakani.
Kumekuwa na ushauri mbalimbali unaotolewa na viongozi wa chama kuanzia ngazi za juu, kati hadi chini kabisa ya namna bora ya kufanya ili kushinda chaguzi hizi. Wanachama wa CCM nao katika nyakati tofauti tofauti nao wamekuwa na maoni na ushauri kadha wa kadha ili kukisaidia chama kuibuka kidedea. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete hakubaki nyuma katika kushauri njia bora ya kufanya ili kukiwezesha chama chake kuibuka kidedea bila kutumia nguvu kubwa na kupata ushindi mapema kabisa.
Hivi karibuni, akiwa kwenye mkutano wa wananchi wa Mkange wakati wa ziara yake jimboni kwake aliwaasa wananchi kuacha kuchagua viongozi kwa kujuana au kwa nguvu ya fedha. Ridhiwani Kikwete alitoa nasaha hizi alipokuwa akihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ni msingi wa kupata viongozi bora watakaokuwa chachu ya maendeleo katika maendeleo yao na nchi kwa ujumla. “Hata kama kuna mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye yeye mwenyewe mnamwona wala hataki mambo hayo, jamii pale inamtaja vizuri, mfuateni na mumwambie kama wewe mwenzetu kila tukikaa kijiweni tunasema kama kuna mtu mzuri wa kutuongoza basi ni yule pale ambaye ni wewe utatuletea mambo mazuri eneo letu. Basi mfuateni na mwambie ili kukisaidie chama chetu. Lakini kutafuta wale marafiki zenu ambao mnauza nao mapori, kutafuta marafiki zenu mnaofanya nao ubadhirifu wa mali za umma, ni kukiingiza chama kwenye mtihani mkubwa sana,” amesema Ridhiwani Kikwete.
Alichosema Ridhiwani Kikwete ni jambo la msingi sana na linapaswa kuzingatiwa na viongozi na wanachama wa CCM kwani mara nyingine wananchi na wanachama wa CCM wamekuwa wakipiga kura za hasira kwa vile tu hakusimamishwa mgombea aliye chaguo la wananchi na hivyo kukidhoofisha chama chao. Wanachama ndiyo wenye chama na si viongozi, hivyo basi wanachama wahakikishe wanakuwa na jicho la tatu la kuangalia nani anafaa kugombea na kupeperusha bendera ya chama na pale inapobidi wamshawishi mwanachama ambaye anao uwezo wa kuongoza lakini ni kama hayupo tayari kugombea.
Mwanachama ambaye huombwa na wananchi baada ya kuona uwezo wake na uadilifu wake mara nyingi huwa mzuri kuliko yule anayejipendekeza mwenyewe kugombea, tena yule anayepita akiwa hiki na kile kwa wananchi (kuhonga) ni hatari zaidi kwani atakalia kutaka kurudisha gharama zake badala ya kuwatumikia wananchi. Mwalimu Nyerere aliwahi kukemea sana mgombea wa aina hii. Ni vyema sisi wananchi ndio tumgharamikie huyo mgombea kama kuna gharama kama za kampeni hata kumshonea suti kwani anakwenda kutufanyia kazi sisi.
Hii yote ni kutengeneza mazingira ya uhakika wa ushindi pindi mgombea huyo atakapopambana na wagombea wa vyama vingine. Katika kusisitiza na kukazia hoja yake, Ridhiwani Kikwete anasema, “Ninaamini viongozi ninyi ambao ni wanachama hamtafanya kosa hilo. Tuleteeni watu ambao tukifika hapa watu wanaendelea na shughuli zao tukisubiri siku ya kupiga kura, tunapiga kura na maisha yanaendelea.”
Naamini tumeelewa alichokisisitiza Ridhiwani Kikwete, cha muhimu ni wananchi kuchagua viongozi bora wanaokubalika katika jamii ambao watakuwa nyenzo ya kufikia maendeleo ya kweli, na hao ndiyo wanaotakiwa katika ujenzi wa Tanzania tuitakayo yenye amani, upendo na maendeleo. Kwa kuazima maneno ya Mwalimu Nyerere, wanachama wa CCM tupendekeze mgombea kwa kila nafasi ambaye mtu akikuuliza unadhani huyu atakuwa kiongozi mzuri, huyu ni mwadilifu, huyu ni mtenda haki, huyu anajua matatizo yetu, jibu litoke moyoni kabisa kabisa na si kwenye ulimi kwamba NDIYO.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.