Na: Zainab Ally Twaha – Mikumi.
TIMU ya Simba Sports Club imeandika historia nyingine nchini ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini baada ya kuzindua jezi zao mpya katika Hifadhi ya Taifa Mikumi iliyopo mkoani Morogoro.
Baada ya uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Augustine Masessa alisema amefurahishwa na kitendo ambacho kimefanywa na timu ya Simba, kwani ni moja ya njia inayotumika kuitangaza hifadhi hiyo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na timu hiyo kutazamwa na mashabiki na watazamaji zaidi ya milioni 50 ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
“Uongozi wa Hifadhi ya Mikumi kwa ujumla wake tumefurahishwa sana na tukio hili la kihistori kwani limeweza kuitangaza vema hifadhi yetu,naushukuru uongozi mzima wa timu ya Simba,naziomba timu nyingine nazo zifanye hivi”alisema Masessa.
Sambamba na pongezi hizo Kamishna Masessa aliongeza kuwa kitendo kilichofanywa na timu ya Simba kimenogesha juhudi za serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan kwa kutangaza vivutio mbalimbali hasa Hifadhi za Taifa zilizopo hapa nchini ikiwemo Mikumi.
Kamishna Masessa alisema kuwa tukio lilofanywa na timu ya Simba mbali na kuitangaza hifadhi ya Mikumi, pia limeonyesha wazi kuwa ndani ya hifadhi hiyo kuna huduma mbalimbali ikiwemo suala zima la michezo ya aina mbalimbali ambapo watu wanaweza kwenda kufurahia mandhari ya hifadhi hiyo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba, Iman Kajula alisema waliamua kwenda kuzindua jezi zao mpya hifadhi ya Mikumi kwani wao wamekuwa mstari wa mbele kutangaza utalii hapa nchini lakini pia walikwenda kukutana na wajina wao ambao ni simba wa sharubu.
Aidha Kajula aliwapongeza mashabiki wa timu hiyo waliyojitokeza katika uzinduzi wa jezi zao ikiwa ni pamoja na wiki yao ambayo kilele chao kitakuwa Agosti 3 mwaka huu ambapo aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kutembelea hifadhi hiyo.
Afisa Habari wa timu hiyo, Ahamed Ally alisema kuwa wameamua Hifadhi ya Taifa Mikumi kuzindua jezi zao mpya kwani hifadhi hiyo ni moja ya hifadhi maarufu hapa nchini lakini pia kuonana na wajina wao kwa jina la Simba wa Mikumi na kwamba kupitia tukio lao hilo la kihistoria umaarufu wa Simba wa Kariakoo na wa Mikumi utaongezeka zaidi hali itakayochochea utalii katika hifadhi hiyo.
Kwa miaka miwili mfululizo timu ya Simba imekuwa ni mhamasishaji mzuri wa utalii katika Hifadhi za Taifa, ikumbukwe mwaka jana 2023 Simba ilizindua jezi zake katika kilele kirefu kuliko vyote Barani Afrika, na kwa mwaka huu wameendelea kutangaza vivutio kwa kuzindua jezi na kutangaza utalii katika Hifadhi ya Taifa Mikumi