Waziri wa Utalii na Malikale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mudrik Ramadhan Soraga Akizungumza katika Mkutano katika kikao cha 46 cha kamati ya Uridhi wa Dunia kinachoendelea Mjini Delhi India.
…………..
Na Mwandishi Maalum, New Delhi, India
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasikitishwa na kiwango cha kampeni ya upotoshaji inayoendelea na tuhuma zisizo na msingi zinazolenga kudhoofisha juhudi za Serikali za kuweka uwiano wa uhifadhi wa urithi, haki za binadamu, maendeleo ya kijamii na kiuchumi na maisha ya wananchi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Hayo ameyasema Waziri wa Utalii na Malikale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, anaongoza Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaohudhuria kikao cha 46 cha Kamati ya Urithi wa Dunia kuanzia tarehe 21 hadi 31 Julai 2024 katika ukumbi wa Bharat Mandapam jijini New Delhi, India. Mkutano huo ulifunguliwa Julai 21 2024 na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa India, Shri Narendra Modi.
Akitoa msimamo wa nchi baada ya kupitishwa uamuzi wa Kamati kuhusu eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mhe. Soraga aliishukuru nchi ya India kwa kuandaa vema kikao cha 46 cha Kamati na Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kuendesha kikao kwa uadilifu na kwa misingi ya kitaalamu.
Waziri Soraga amekieleza kikao cha Kamati kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kuweka kumbukumbu wazi na kukanusha dhana ya madai ya kuondolewa kwa nguvu kwa raia wake kutoka Ngorongoro.
Waziri huyo amesema Ili kuweka mambo katika muktadha, alifafanua, baada ya Mfumo wa Matumizi Mseto wa Ardhi kushindikana kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya binadamu na wanyamapori, ongezeko la watu na mifugo, kuenea kwa magonjwa ya wanyama pori yanayowapata wanadamu, kupungua kwa ushoroba wa wanyamapori na malisho, ukosefu wa vyanzo vya maji salama na usafi duni wa mazingira na azma ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya raia wake, maafikiano yalifikiwa kupitia mchakato shirikishi na wa uwazi yaliyopelekea mpango wa kuhama kwa hiari kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Aidha amesema Kamati ya Urithi wa Dunia hukutana kila mwaka na ina jukumu la kusimamia masuala yote ya Urithi wa Dunia na kuamua kuhusu maeneo ya kuingizwa katika orodha ya Urithi wa Dunia.
Wakati wa mkutano huo, Taarifa za Hali ya Uhifadhi wa Maeneo ya Urithi wa Dunia, mapendekezo ya kuingiza maeneo mapya kwenye orodha ya Urithi wa Dunia, Msaada wa Kimataifa na Matumizi ya Mfuko wa Urithi wa Dunia yanajadiliwa. Kwa sasa, kuna Maeneo 1199 ya Urithi wa Dunia katika mataifa 168 kati ya 195 Wanachama wa UNESCO.
Mkutano huo unahudhuriwa na zaidi ya wajumbe 2,000 wa kimataifa na kitaifa kutoka zaidi ya nchi 150. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina maeneo saba ya Urithi wa Dunia katika orodha hiyo ambayo ni, Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Michoro ya Miambani ya Kondoa, Pori la Akiba Selous na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Waziri Soraga alisisitiza msimamo thabiti wa serikali kwamba hakuna watu wa asili mahususi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inatambua kuwa kuna jamii zenye mahitaji maalum kama vile Wahadzabe na inahakikisha kwamba haki zao za kiraia, kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni zinakuzwa na kuheshimiwa. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongozwa na utawala wa sheria na misingi ya utawala bora, imeweka haki za binadamu mbele wakati ikishughulikia changamoto zilizopo katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Serikali ilialika Ujumbe wa Ushauri wa UNESCO kwa Hifadhi ya Ngorongoro mnamo Februari 2024 na taarifa yake inakamilishwa. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina dhamira ya kushirikiana kwa karibu na Kituo cha Urithi wa Dunia na nchi nyingine wanachama wa UNESCO katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Soraga aliuambia mkutano huo kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuzingatia haki za binadamu sambamba na kusawazisha uhifadhi wa urithi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi na maisha ya watu wake katika Hifadhi ya Ngorongoro