Mwamvua Mwinyi,Pwani
Julai 25, 2024
SERIKALI Mkoani Pwani, imeonya watu wasio wazalendo ambao wamekuwa wakisambaza kwenye mitandao ya kijamii taarifa za uongo kuhusiana na kutekwa kwa watoto kitendo ambacho kinasababisha taharuki kwa wazazi na jamii.
Vilevile imekemea, watu wanaojihusisha na utekaji watoto, kuacha tabia hiyo kwani atakaebainika atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakar Kunenge ametoa onyo hilo Kibaha Mkoani Pwani kwenye maadhimisho ya siku ya mashujaa.
Ameeleza vyombo vya dola, Jeshi la polisi mkoa wa Pwani vimejipanga kudhibiti na vina vina weledi mkubwa, Teknolojia ya kutosha kubaini watu wanaojirekodi na kusambaza uongo.
Kunenge alifafanua kuwa, wanajua kila kinachoendelea hivyo wanaomba ushirikiano kwa wananchi kuzuia na kutoa taarifa za vitendo vya aina hiyo kwenye maeneo yao.
Aliomba endapo jamii ikibaini wauaji wa wenye ulemavu wa ngozi, utekaji watoto, mauaji, vitendo vya unyanyasaji watoto na wanawake wafichue vitendo hivyo ili watuhumiwa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria.
“Kuna sura mbili katika ya masuala ya utekaji, kuna ukweli yapo matukio ya utekaji ambayo tunakemea kwa nguvu zote kwa wanaojihusisha”
“Lakini kuna sura nyingine kwa baadhi ya watu wanaokwenda na upepo wa matukio hayo ambao wanaojirekodi kusema uongo kuwa kuna watoto wametekwa, Tuzuie vitendo hivi,tushirikiane kutoa taarifa kwa watu wanaoleta taharuki ,lakini tukiwabaini tusijichukulie sheria mkononi “”alisisitiza Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa alilipongeza Jeshi la polisi mkoa wa Pwani kwa kuwakamata baadhi ya watu waliojirekodi klipu ya uongo kwamba kuna watoto wametekwa huko Vigwaza hali ambayo ilisababisha hofu na taharuki.
Kunenge alisema,Jeshi hilo linaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa kina wenye kufanya vitendo hivyo ili kubaini dhamira yao.
Nae Mchungaji Julius Shemkai,ambae pia ni Mwenyekiti mwenza wa kamati ya amani mkoani Pwani, alikemea vitendo vya utekaji watoto wasio na hatia.
Wakati huo huo, Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani humo, Pius Lutumo alieleza Jeshi hilo linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuzusha ,kurekodi na kusambaza taarifa ya uongo kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna gari aina ya Noah inayopita maeneo mbalimbali na kuwateka watoto wadogo.
Aliwataja watuhumiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwa Zoka Shomari Tengeneza Zinga (64) ,Aishi Ally (32), Alphonce Temba (34) na Paul Didasi Mwanilezi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Vigwaza.
Lutumo alibainisha ,watu hao walitanabaisha kuwa watoto wawili wa Shule ya Msingi Vigwaza wametekwa jambo ambalo si kweli.
“Taarifa hizi zilienea kwa haraka hadi shule ya Msingi Mtongani iliyopo Mlandizi Wilayani Kibaha na kuleta taharuki kwa wazazi, walimu na watoto wa shule hiyo ambapo mzazi Zaituni Idd Shabani, alielezwa kuwa mtoto wake aitwaye Isimaiya Zuberi (6) shule ya Msingi Mtongani kuwa ni miongoni mwa watoto waliotekwa”