Mwamvua Mwinyi, Pwani
Julai 25, 2024
SERIKALI Mkoani Pwani, imesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa shujaa katika kuendelea kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya mwendo kasi hadi kufikia hatua ya kuanza usafirishaji.
Imempongeza kwa hatua ya kuzindua treni ya mwendokasi ya (SGR) kuanzia Dar es salaam kwenda Dodoma kwani ni tukio la kishujaa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge ametoa pongezi hizo wakati wa kuadhimisha ya Kumbukumbu ya Mashujaa kimkoa yaliyofanyika viwanja vya ofisi ya mkoa huo ,Julai 25,mwaka huu.
Kunenge alieleza ,jambo hilo ni kubwa na la kihistoria ambalo Rais ameweka rekodi ya usimamizi mzuri wa utawala wake.
Mkuu huyo wa mkoa, alifafanua baadhi wapinga uchumi walijaribu kuhujumu miradi mikubwa ya kitaifa lakini kwa utendaji kazi wa Rais wameshindwa.
“Wakati tukiendelea kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa wetu, Tumuombee Rais kwa kazi hii kubwa anayoifanya kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inasonga mbele, Tumeshuhudia utekelezaji wa mradi huu wa reli ya SGR na bwawa la uzalishaji umeme kule Stigo Rufiji ,”alifafanua Kunenge.
Kunenge aliomba jamii kuendelea kuwaenzi mashujaa wetu waliopigania Taifa letu ,ambao wameshafariki na ambao bado wapo hai.
Hata hivyo, Kunenge aliwaomba wananchi Mkoani Pwani ,kujitokeza agost mosi katika baadhi ya vituo ambavyo Rais Samia atasimama kusalimia kwenye reli ya SGR inayopita Mkoani humo.
Nae Sheikh Saidi Chega ,aliliomba Taifa kuendelea kumuombea Rais Samia Suluhu na kumuunga mkono kwa kazi kubwa anayoifanya kuinua uchumi wa nchi.
Chega pia alikemea vitendo vya uhalifu ,mauaji na ukatili kwa watoto ili kulinda amani na usalama.
Siku ya Mashujaa huadhimishwa 25,Julai kila mwaka ambapo kipindi cha nyuma siku hii ilikuwa ikiadhimishwa pamoja na siku ya majeshi septemba mosi ikiwa ni siku ambayo ilianzishwa Jeshi la wananchi septemba 1,1964.