Mbunge wa jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa,akisalimiana na baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo kabla ya kuanza kwa kikoa cha Halmashauri kuu ya wilaya iliyofanyika katika Ukumbi wa shule ya Sekondari Dkt Samia Suluhu Hassan mjini Namtumbo.
Baba lishe Said Mohamed kushoto mkazi wa mtaa wa Rwinga wilayani Namtumbo,akipokea jiko la gesi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa yaliyotolewa na Mbunge huyo ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa jimbo hilo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Peter Ndomba kushoto,akikabidhi mitungi 300 ya gesi kwa Mbunge wa jimbo la Namtumbo Vita Kawawa kwa ajili ya kugawa kwa Mama na Baba lishe ikiwa ni kutekeleza mpango wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Peter Ndomba,akizungumza na Mama na Baba lishe pamoja na madiwani wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo wakati wa kukbidhi majiko 300 ya gesi yenye thamani ya Sh.milioni 25.5 yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa ili kuhamasisha jamii kuhusu matimizi ya nishati safi ya kupikia.
……………….
Namtumbo
Na Mwandishi Maalum,
Namtumbo
MBUNGE wa jimbo na Namtumbo Vita Kawawa kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd,wamekabidhi majiko 300 ya Gesi yenye thamani ya Sh.milioni 25,500,000 kwa Mama na Baba lishe wanaouza chakula katika maeneo mbalimbali wilayani Namtumbo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi majiko hayo Kawawa alisema,lengo ni kuhamasisha kundi hilo na jamii kwa ujumla, kuanza kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa ambayo yamesababisha uharibu mkubwa wa mazingira.
Alisema,ametoa majiko hayo ili kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania,na kuwaomba Mama na Baba lishe kumsaidia Rais Samia katika suala zima la utunzaji mazingira.
Aidha alisema,majiko hayo yametimiza ndoto za muda mrefu za kuwapatia wananchi wa Jimbo la Namtumbo hususana Mama na Baba lishe wanaotumia kiasi kikubwa cha kuni na mkaa kupika chakula kwa ajili ya biashara na familia zao.
“Huu ni mwanzo tu kwa wananchi wa Namtumbo,kwani dhamira yangu nataka kuhakikisha kila mjasiriamali anayeuza chakula anatumia nishati safi badala ya kuendelea na matumizi ya kuni na mkaa”alisema Kawawa.
Ameishukuru Kampuni ya Oryx Gas kwa kusimamia mpango wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa,bado jamii ina nafasi kubwa ya kujirekebisha kwa kuacha kutumia kuni na mkaa ili kulinda mazingira katika maeneo yao.
“Tunapozungumzia suala la nishati safi ya kupikia tunamzungumzia moja kwa moja Mheshimiwa Rais Samia,suala la nishati safi ni ajenda yake mwenyewe,kwa hiyo sisi wananchi na viongozi hatuna budi kumsaidia, tunawashukuru wenzetu wa Oryx Gas kwa kutupatia majiko haya”alisema Kawawa.
Kwa upande wake meneja miradi wa nishati safi ya kupikia Peter Ndomba aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Benoit Araman alisema,kwa muda mrefu wamekuwa wanajivunia kuwezesha makundi mbalimbali ya kijamii kupata nishati safi ya kupikia.
Alisema,kupika kwa Gesi ya Oryx kuna maanisha kuboresha afya za Watanzania hususani akina Mama kwa kuepuka kuvuta moshi mbaya unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa wakati wa kuandaa chakula cha familia.
Kwa mujibu wa Ndomba,matumizi ya nishati safi yanasaidia kuokoa maisha ya watu na kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Alisema,takwimu zinaonyesha zaidi ya watu 33,000 hapa nchini wanapoteza maisha kila mwaka kwa kuvuta moshi na chembechembe zinazotokana na matumizi makubwa ya kuni na mkaa.
Naye Katibu Tawala wa wilaya ya Namtumbo Fransis Mgoloka,amewataka wakazi wa wilaya ya Namtumbo kuhakikisha wanaanza kubadili mfumo wa maisha kwa kutumia nishati safi na mbadala ili kulinda mazingira badala ya kuendelea kutumia kuni na mkaa.
“Sisi ni sote ni mashuhuda,unaposema mabadiliko ya tabia ya nchi inawezekana watu wengi hawafahamu, lakini suala hili limekuwa likijadiliwa sana, unapoona ongezeko kubwa la joto na mvua inanyesha kupita kiasi hayo ndiyo mabadiliko ya tabia ya nchi na kwa asilimia kubwa yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira”alisema.
Mfanyabiashara wa chakula kutoka mtaa wa Rwinga Hadija Mussa alisema,majiko hayo yatasaidia kuandaa chakula kilicho bora na wateja watapata huduma kwa haraka ikilinganisha na hapo awali walipokuwa wanatumia mkaa na kuni.