Na Sophia Kingimali
HISTORIA imeandikwa baada ya Shirika la Reli Tanzania kutimiza agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuanza safari za treni ya kisasa ya Umeme(SGR) kuanzia Dar es Salaam-Dodoma.
Pia, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa ameshindwa kuzuia furaha yake kuiona safari hiyo ikianza rasmi kwa zaidi abiria 900 wakiwa ndani mabehewa 14 ikiwa ni siku yake maalumu ya kuzaliwa kwa kutimiza miaka 50.
Vilevile safari za SGR Dar -es Salaam-Dodoma zinatajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Dk. Samia hivi karibuni.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 25,2024 katika uzinduzi wa awali, Kadogosa amesema amefurahi sana kuona maagizo ya Rais Dk. Samia kuyikitimia.
“Tunashukuru sana leo ni siku ya furaha kwa TRC kwa kutekeleza maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya mwaka jana wakati tunafunga mwaka maagizo yake ni kufikia mwishoni Julai, tuwe tumeanza treni ya kutoka Dar es Salaam-Dodoma,” amesema.
Kadogosa amesema safari hiyo wameisubiri kwa muda mrefu hivyo wameanza lakini mwenye reli mwenyewe ambaye ni Rais Dk. Samia hivi karibuni atauzindua rasmi.
“Sisi tumeanza katika hali ya kawaida kama tulivyoanza Dar es Salaam-Morogoro lakini uzinduzi rasmi tutautangaza rasmi,” amesema.
Amesema treni hiyo imebeba abiria zaidi ya 900 katika mabehewa yote 14.
Kadogosa amesema treni hiyo inaweza kubeba hadi mabehewa zaidi ya 20 lakini huwa wanaangalia kasi ya uendeshaji kwani ukibeba mabehewa zaidi ya 14 huwa inapungua.
“Tunawashukuru Watanzania kwa mwitikio wao, hii treni ipo ‘full’ na kuna watu wengine wamekosa tiketi kwani Daraja la biashara na kawaida yamejaa sasa na treni ya Dodoma -Dar es Salaam imeondoka saa 11.30 hivyo tuna treni pia ya kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam,” amesema.
Amesema nauli daraja la kawaida Dar es Salaam- Dodoma ni sh.31,000 huku Morogoro ikiwa sh.13,000.
Kwa upande wake Mchungaji Kanisa la Anglikana Chanika, Christina Mulila amesema amefurahi kusafiri na treni kwani ni mara ya kwanza kwake.
“Ninashukuru kwa urahisi wa usafiri tuliorahisishiwa, gharama ya muda na ubora wa treni, hivyo nimeona niwe wa kwanza kusafiri kwa treni hii kufika mahali husika kwa muda muafaka na usafiri bora zaidi,” amesema.
Aidha amewasihi Watanzania watumie usafiri huo kwa sababu ni bora, salama na rahisi lakini pia ni uzalendo.
Zakaria Nundi, mkazi wa Kigamboni, amesema anajisikia furaha kujiunga na wenzake kwenda Dodoma hivyo amewataka Watanzania wautumie kwani ni wa uhakika na salama lakini pia ni sehemu ya utalii.
“Ninaamini ni usafiri mzuri kwani nimeona mandhari yake ni mazuri na yamependeza sana, kwa kweli kazi ya serikali yetu tumeiona na inafanya kazi vizuri sana,” amesema.
Juni 14, mwaka huu, TRC walianza safari ya treni hiyo kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na kuwa na mwamko mkubwa kwa Watanzania hususani wakazi wa Dar es Salaam-Morogoro.