![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2024/07/Screenshot_20240724-214038-1024x642.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2024/07/Screenshot_20240724-213938-1-1024x640.jpg)
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga kulia,akiangalia mbegu za mazao hususani mahindi kwenye uzinduzi wa kampeni ya Uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima uliofanyika katika Hotel ya One Pasific mjini Mbinga.
……………….
MbingaMATUMIZI ya mbolea hapa nchini,yameongezeka kutoka wastani wa tani 363,599 katika msimu wa kilimo 2021/202 hadi kufikia tani 840,714 kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania Joel Laurent amesema hayo jana,wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha usajili wa wakulima na matumizi sahihi ya mbolea uliofanyika wilayani Mbinga.
Amesema,mkoa wa Ruvuma ambao ni kati ya Mikoa ya kimkakati ya uzalishaji wa chakula hapa nchini, kwa miaka ya karibuni umeongoza kwa matumizi ya mbolea ambapo msimu 2022/2023 Mkoa huo ulitumia zaidi ya tani 83,472.
“katika msimu 2023/2024 mkoa wa Ruvuma umetumia tani 100,000,hivyo kuendelea kuwa kinara kwa matumizi ya mbolea na kuwa miongoni mwa mikoa tegemezi katika uzalishaji wa chakula hapa nchini”amesema.
Laurent alitaja mikoa inayofuatia kwa matumizi ya mbolea ni Njombe tani 75,358,Mbeya tani 75,252,Songwe tani 71,230 na mkoa wa Iringa ambao umetumia tani 44,214.
Ameongeza kuwa,hapa nchini kuna mbolea za viwandani na mbolea za asili ambazo zinatumiwa na wakulima,lakini changamoto ni matumizi kidogo ya mbolea kwa baadhi ya maeneo kunatokana na dhana potofu kwamba mbolea inaharibu ardhi na baadhi ya wakulima kukosa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea”alisema Laurent.
Amewakumbusha wakulima umuhimu wa kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao kwenye mashamba yao kwani unasaidia kurutubisha,kuboresha afya ya udongo na kuzalisha mazao kwa wingi katika eneo dogo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga alisema,sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa Tanzania na inaajiri takribani theluthi mbili ya nguvu kazi ya Taifa na inachangia asilimia 65 ya malighafi za viwandani,asilimia 100 ya usalama wa chakula na zaidi ya asilimia 26 ya pato la Taifa.
Kapinga amesema,katika mazingira ambayo kilimo ndiyo sekta ya uchumi,maendeleo ya mwananchi na Taifa kwa ujumla yanategemea zaidi ufanisi katika sekta hiyo.
Amesema,Serikali ya awamu ya sita imedhamira kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya wizara kutoka takrbani Sh.bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh.trilioni 1.24 kwa mwaka 2024/2025.
Amewataka wakulima hapa nchini wakiwemo wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma,kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kujisajili katika mfumo wa kidijitali kupitia Ofisi za Watendaji wa vijiji na mitaa.
Naibu Waziri Kapinga alisema,kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali kutawaweza wakulima kununua mbolea kwa gharama nafuu,kuongeza uzalishaji,kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Ametaja faida nyingne kwa wakulima kujisajili kwenye mfumo wa kidijitali,ni kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazotumika kuweka mipango ya kuwaendeleza wakulima,sekta ya kilimo na kupata huduma za ugani,taarifa za masoko na huduma za kifedha kupitia kanzidata.
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Jumanne Mankhoo,ameipongeza mamlaka ya udhibiti wa ubora wa mbolea kwa kusimamia vema upatikanaji wa pembejeo za ruzuku iliyosaidia kupatikana kwa wingi na kwa urahisi katika meneo mengi ya mkoa huo.