*Waipongeza Serikali ya Rais Samia kuboresha huduma za jamii
*Waomba kujengewa Barabara kusafirisha mazao
*Dkt. Biteko aagiza kukamilishwa, kutumika Zahanati Kijiji Ilyamchele
*Awahakikishia ukarabati wa Barabara ipitike nyakati zote
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Wananchi wa Kijiji cha Ilyamchele, Kata ya Namonge Wilayani Bukombe wameipongeza Serikali kwa kuboresha huduma mbalimbali za jamii katika Kata hiyo huku wakishukuru mamilioni yaliyoelekezwa katika uboreshaji wa huduma hizo.
Pongezi hizo zimetolewa mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko alipofanya ziara kuhutubia wananchi katika mkutano uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa kata ya Namonge.
Akizungumza katika Mkutano huo, Diwani wa Kata ya Namonge Mhe. Mlalu Bundala amesema serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha huduma za jamii zinaboreshwa na kuwawezesha wakazi wa Kata ya Namonge inapanda hadhi.
Amezitaja huduma zilizoboreshwa ni pamoja na matumizi ya zaidi ya shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kujenga madaraja ya awali katika shuele mbili za msingi na sekondari ambazo kwa pamoja zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.31, Ametaja miundombinu mingine kuwa ni uchimbaji wa visima 5 vya maji chini ya pango wa Rais Samia kumtua mama Ndoo, Miradi mingine iliyoelezwa kuboreshwa ni katika sekta ya nishati ya umeme.
Mhe. Bundala amesema, Wananchi wa Kata hiyo wanaomba huduma ya Zahanati katika Kijiji cha Ilyamchele baada ya wananchi kuchangia nguvu zao lakini kituo hicho kushindwa kufanya kwa kushindwa kukidhi viwango vinavyokubalika kwa huduma hizo.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kuboresha huduma za jamii na kuongeza kuwa kuna uongozi bora unaowezesha utekelezaji wa majukumu kulingana na maono ya viongozi ngazi za juu.
“ Pokeeni salamu za Kiongozi wetu Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amenituma niwafikishie salamu zake za upendo, Nilipomuomba kuja kusalimia aliniruhusu na kuahidi kuwa siku za karibuni atakuwa na ziara Mkoani Geita na akifika atapata fursa ya kuwatembelea wananchi wa Kata hii ya Namonge” amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko akijibu hoja mbalimbali zilizowasilishwa, ameelekeza kufanyika kwa ukarabati wa Zahanati ya Kijiji hicho ili kumaliza kilio cha wakazi wa eneo hilo “ Ukarabati wa Zahanati hii uanze mara moja na kuahidi kutoa vifaa vinavyopungua ili huduma za afya zianze kutolewa kijijini hapo haraka iwezekanavyo.
Amewataka wananchi wa Kata hiyo kuhakikisha wanawapeleka Watoto wao shule na wale wanaoleta ukinzani dhidi ya maelekezo hayo waripotiwe katika mamlaka za ngazi husika ili kutafuta suluhu ya tatizo hilo.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amelazimika kusimama katika eneo la Makao Mkuu ya Kata ya Namonge ili kuwasilikiliza wananchi waliozuia msafara wake wakiomba kusikilizwa na Mbunge wao kuhusu miundombinu ya Barabara. Wananchi hao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali waliomba kujengewa Barabara katika kiwango cha lami ndani ya Wilaya ili waweze kutumia Barabara hiyo kusafirisha mazao yao kutoka mashambani.
Akizungumzia hoja hiyo, Dkt. Biteko amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itaendelea kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu ili iweze kupitika wakati wote kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha huku akitoa mfano wa uboreshaji wa miundombinu katika kipindi cha miaka michache iliyopita.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella ametumia mkutano huo kutumia fursa ya uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kupata sifa ya kuwachagua viongozi wao ngazi ya Rais, wabunge na madiwani ifikapo mwaka 2025.
“Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini pia mwakani tutakuwa na uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, Tarehe 5 hadi 11 Agosti mwaka huu tutahitajika kujiandikisha ili kuwachagua viongozi tunaowataka muda utakapofika.