Agizo limetolewa kwa Uongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kuchukua hatua za haraka kukamilisha ujenzi wa Zahanati iliyopo Kitongoji cha Jasini, Kijiji cha Mahandakini mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akisikiliza kero za Wananchi kupitia Mkutano wa hadhara.
Katika mkutano wake huo, Balozi Dkt Batilda Burian amesema, Kijiji hicho ni cha mkakati hivyo kuna kila sababu ya huduma za msingi kuimarishwa hatua ambayo iyawezesha kuondoa kero kwa wananchi wa eneo hilo.
“Kabla ya mwisho wa mwaka huu Zahanati iwe imekamilika, pia umeme kutokana na unyeti wa eneo hili, Pia barabara na maji vifanyiwe kazi kuchimbwe hata visima wakati taratibu nyingine zikifanywa” alisema Balozi Dkt Batilda Burian huku akiahidi kuchangia Shilingi milioni tano (5).
Akionesha msisitizo wa upatikanaji huduma za msingi, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza mhandisi wa maji kufika kwenye eneo hilo ili kufanya utafiti wa kupatikana maji yasiyokuwa na chunvi, akisema haipendezi huduma kukosekana.
Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa Zahanati hiyo amesema kwamba,usaidizi mkubwa wa masuala ya afya wamekuwa wakiupata kutoka nchi jirani ya Kenya.
Alisema, kunapotokea dharura za kiafya akitolea mfano Wajawazito wamekuwa wakienda eneo la upande wa Kenya ambapo ni umbali wa takribani Kilomita moja huku la Tanzania kwenye huduma ni Kilomita 10.
Huduma nyingine zilizo lalamikiwa ni ukosefu wa nishati ya umeme ambapo Wavuvi wamejikuta Samaki wao wakioza kutokana na kushindwa kuwahifadhi.
Changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama,barabara na mifugo kushambulia mazao yao mashambani ambapo baadhi ya wafugaji wanashindwa kudhibiti mifugo yao kwa kuicha kushambulia mazao ya wakulima.
Ally Suleyman alisema, maeneo wanayotumia kwa Uvuvi wa Samaki yamechukuliwa na watu wa Kenya, jambo ambalo limechangiwa na kutotqmbulika kwa mipaka ambapo wavuvi hukamatwa na kupelekwa nchini Kenya kwa ajili ha kuhukukiwa.