Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ameuagiza Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania ukutane na kuzungumza na baadhi ya wasanii waliokopa fedha awali kupitia mfuko huo na kushindwa kurejesha kwa wakati kabla ya kuanzishwa kwa utararibu mpya wa kutumia benki kukopesha wasanii ili kuangalia namna bora ambayo wanufaika hao watarejesha mikopo hiyo akisisitiza kuwa hakuna mkopo utakaofutwa.
Mhe. Mwinjuma ametoa agizo hilo leo Julai 23 2024 Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na wanufaika wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo pia ameelekeza itafutwe namna bora ambayo itasaidia mikopo yote kurejeshwa.
“Kila fedha iliyotolewa na Mhe. Rais kwa ajili ya kukopesha wasanii lazima irudi, mtu yeyote, aliyechukua anatakiwa kurudisha ili wengine wanufaike, tutakachofanya ni kuangalia utaratibu rahisi utakaowezesha baadhi mlioshindwa kurejesha kwa wakati mrejeshe”
“Namuagiza Mtendaji Mkuu wa Mfuko akae nanyi, naomba mtoe ushirikiano, muangalie namna ambayo itawawezesha kurejesha mikopo yenu mathalani kupunguza kiwango cha marejesho msingi fedha yote irejeshwe” amesisitiza Mhe. Mwinjuma.
Aidha, amefurahishwa na mwenendo wa marejesho tangu benki zilipoanza kusimamia suala hilo akieleza kuwa utaratibu huo umerahisisha urejeshaji wa mikopo hivyo utaendelea kutumika.
Mhe Mwinjuma ameongeza kuwa Mfuko huo unaendele kufanya tathmini na kuangalia namna ambayo itawezesha kukopesha wasanii hata kwenye miradi isiyohusiana na Sanaa akifafanua kuwa Bajeti ya mfuko huo imeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 1.6 mwaka 2023/24 Hadi bilioni 3.0 kwa mwaka 2024/25 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 187.5.