Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akikagua zoezi la usajili katika mfumo wa kielektroniki wa kadi za uanachama wa CCM na kutoa maelezo kwa Watendaji wa CCM kuendesha kwa kwa ufanisi zoezi hilo huko Tawi la CCM Muembeshauri Unguja.
…………………
Na Mwandishi Wetu,Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, amewasihi wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kujisajili katika mfumo wa kielektroniki wa kadi za uanachama wa CCM.
Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kuangalia na kukagua zoezi hilo linalofanyika katika matawi mbalimbali nchini alipotembelea matawi ya CCM ya Wilaya ya Mjini Kichama Unguja.
Alisema usajili huo ni muhimu kwa kila mwanachama anatakiwa kusajiliwa katika mfumo wa kielektroniki wa kadi hizo ili kutambulika katika mfumo huo kwa dhamira ya kupata haki mbalimbali za uanachama.
Dkt.Dimwa, alifafanua kuwa kila mwanachama aliyekuwa na kadi ya zamani ya gamba ambaye bado hajasajiliwa katika mfumo huo anatakiwa kwenda katika tawi lake la Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya kujisajili.
“Wito wangu kwa wanachama wote tuendelee kuhamasishana kushiriki zoezi hili la usajili hasa kwa wanachama wote wenye sifa za kutimiza umri ambao wana kadi za zamani na wengine hawana hata hizo kadi waende katika matawi yetu kwa ajili ya usajili huu”, alisema Dkt.Dimwa.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, aliwasisitiza watendaji wa CCM wanaosimamia zoezi hilo la usajili kuhakikisha kila mwanachama anapata haki hiyo ya kusajiliwa kwa wakati na taarifa zao zinahakikiwa kwa usahihi kabla ya kuingizwa katika mfumo huo.
Pamoja na hayo alisema kuwa CCM inaendeleza malengo yake ya kujiendesha katika mfumo wa sayansi na teknolojia ili kurahisisha masuala mbalimbali ya kiutendaji,kisiasa na kiuchumi yenye maslahi kwa wanachama wote nchini.