Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule amewataka wakazi wa Magomeni Kota kutokukubali kuhadaiwa na watu wachache wenye nia ovu na nyumba hizo ambapo ameahidi serikali kuwashughulikia pindi watakapo wabaini.
Akizungumza leo Julai 22,2024 kwenye kikao na wananchi wa magomeni Kota kuhusu kero mbalimbali wanazokutana nazo ikiwemo ukatikaji wa maji amesema amekuwa akipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wakazi wa eneo hilo ambapo changamoto kadhaa wameshazishughulikia.
Amesema dhamira ya serikali ni kuwawekea mazingira mazuri wananchi wake.
“Dhamira ya serikali ya awamu ya sita ni kuona wananchi wake wanakaa kwenye mazingira mazuri lakini pia mji unapangwa vizuri uwekezaji mkubwa umefanywa kwenye nyumba hizi hivyo niwaombe wananchi msikubali kurubuniwa na watu wachache”,Amesema.
Ameongeza kuwa serikali iliamua kufikia maamuzi ya kuijenga magomeni Kota na kuwapa wananchi(wakazi wazawa wa eneo hilo)ili kuwapa mazingira bora.
“Changamoto nyingi zinazotokea hapa mimi nazijua kuna watu wanawashawishi wengine wanauza nyumba zao pesa unayopewa hata kama ni milioni 25 bado haina thamani ya nyumba uliyopewa na serikali msidanganyike mkauza nyumba hizi.
Nao baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameiomba serikali kuwasaidia kupata nyumba zao kwenye eneo hilo kwani wamekumbwa na sintofahamu ya kutokabidhiwa nyumba zao licha ya kuwa tayari walishafanyiwa tathmini.
Wamesema tathmini walifanyiwa kwa awamu zote mbili lakini kamati iliachiwa jukumu hilo na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya kinyume.
“Kamati imefanya kinyume na maneno ya Rais wakati akikabidhi nyumba hizi kwani watendaji wameenda kinyume kwani wamekuwa wakiziuza nyumba hizo ambapo ni kinyume na utaratibu”,wamesema wananchi hao akiwemo Bi.Amina Adam mkazi wa Magomeni Kota.