Na Neema Mtuka
Rukwa
Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia weredi na miiko ya kazi zao na kuandika habari za kijamii zaidi ili wananchi waweze kupata habari zenye kuleta manufaa kwao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Focus Mauki ambaye ni Mkuu wa kitengo Cha mawasiliano serikalini wakati akitoa mafunzo kwa wanachama wa Club ya waandishi wa habari Mkoa wa Rukwa.
Mauki amesema waandishi wa habari wakiandika habari za ukweli na zenye tija zitawafikia wananchi na kuondoa sintofahamu za habari zisizo na ukweli.
Aidha Mauki amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanapata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu utendaji wa ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ( CAG).
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kitengo Cha huduma za kiufundi Happy Mlingi amesema Moja ya shabaha yao ni kuhakikisha Wana wajengea uwezo wadau mbalimbali ili wawe na uelewa wa kutosha na kufanya kazi kwa misingi ya uwajibikaji.
Pia Mlingi amesema kuwa ofisi inaimarisha masuala ya rasilimali watu na taaluma kwa watumishi.
Mauki amesema ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) imejidhatiti katika kuimarisha masuala ya usimamizi utawala na maadili pamoja na kuwa na mawasiliano kati ya ofisi hiyo na wadau wengine.
Naye Mwenyekiti wa Club ya waandishi wa habari Mkoa wa Rukwa Nswima Ernest ameishukuru ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa kuwapa mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi na kuomba kuwa na mahusiano ya karibu pindi wanapohitaji msaada kutoka ofisi hiyo.
Awali akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Libori center Manispaa ya Sumbawanga Mkaguzi Mkuu wa nje (CEA) Mkoa wa Rukwa Thomas Lumbillah amesema ataendeleza ushirikiano ili kufanya kazi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) kuwa nyepesi na kuleta maendeleo chanya na kudhibiti uvujaji wa fedha.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Daudi Anubi ameishukuru ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari kwani imewapa fursa ya kujua kazi zake lakini pia wamepata nafasi ya kutoa maoni yao.
Anubi Amesema jambo hilo ni zuri na lina chochea ofisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kuendelea kufanya maboresho na kufanyia kazi baadhi ya mapungufu katika ofisi yake.