WANAWAKE Wafanyabiashara, wajasiriamali na vijana nchini wameshauriwa kutumia fursa ya soko la huru la Afrika Mashariki ; ‘East Africa Commercial & Logistics Center (EACLC,) kwa kupata fursa za masoko pamoja na uhakika wa bidhaa kutoka kwa wazalishaji wenye viwanda kupitia soko hilo linalojengwa Ubungo jijini Dar es Salaam na kutarajiwa kuanzia biashara Oktoba Mosi mwaka huu
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kufungua mkutano ulioratibiwa na EACLC kwa kushirikiana na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC,) na kuwakutanisha vijana, wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali Raisi wa TWCC: Chama Kikuu cha Kuendeleza Biashara za Wanawake Wajasiriamali Tanzania Mercy Sila amesema; wamekutana na wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali na kujadili kuhusu fursa mpya ambayo serikali imeileta nchini.
Amesema soko huru la Afrika Mashariki ni fursa kubwa kwa watanzania hususani wanawake ambao kwa sasa wamekuwa kinara katika masuala ya biashara.
“Ni soko kubwa ambalo limejengwa mahususi kwa ajili ya bidhaa zinazotoka China na tulipata fursa ya kukutana nao na wakatueleza ni kwa namna gani wanawake au wafanyabiashara wa Tanzania wanaweza kutumia fursa hii…..Na sisi tumeona hii ni fursa nzuri na kwa haraka tumewaita wanawake wafanyabiashara na vijana ili tuweze kushiriki fursa katika soko hili.” Amesema.
Ameeleza kuwa, kupitia soko hilo wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali watapata fursa ya kupata taarifa za viwanda vya bidhaa wanazohitaji na kuvitembelea pamoja na namna ya kusafirisha bidhaa zao jambo litakalorahisha biashara.
“Fursa hii inawafaa sana wanawake hapa kutakuwa na bidhaa za jumla na rejareja na TWCC tumekuwa tukiwaunganisha wanawake na vijana katika masoko ya China lakini fursa hii ni muhimu na wanawake wengi watanufaika na tutaendelea kuwahamasisha wanachama wa TWCC, wajasiriamali na wanawake wote kwa ujumla tushiriki fursa hii ambayo imeletwa nchini kwetu na Serikali inaitambua hili.” Amefafanua.
Kwa upande mwakilishi wa soko la EACLC Chacha Mwita amesema wamekutana na TWCC ili kuwapa fursa za soko hilo kubwa la kisasa ambalo lina sehemu mbili ambazo ni jengo dogo ni kwaajili ya taasisi za fedha na jengo kubwa maalum kwa biashara zote.
Amesema soko hilo litaanza shughuli zake rasmi Septemba 30 na kuzinduliwa rasmi Oktoba Mosi kwa wafanyabiashara kukabidhiwa funguo na kuingia katika maduka yao na kueleza kuwa katika soko hilo watanzania watafanya biashara pale na wataunganishwa na wazalishaji wa bidhaa wanazohitaji.
“Tunawapa wanawake kipaumbele ili waweze kufanya makubwa zaidi…Changamoto tuliyonayo Tanzania ni kuhitaji bidhaa lakini hatujui nani tukutane naye kwa hilo….Soko hili limekuwa ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara wa Tanzania Afrika, China na Nchi nyingine ili wafanye biashara kwa ukubwa.
Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo na kati wa Mwanga Hakika Bank Mwinyimkuu Ngalima amesema, katika jitihada za kuhakikisha wanawakomboa wanawake kiuchumi wanaangalia fursa na utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kwa kushirikiana na TWCC ili kutimiza malengo yao yenye tija kwa jamii kwa kuhakikisha wanapata elimu, mikopo ya riba nafuu pamoja na kutoa elimu ya fedha na kuweka akiba ili kukuza na kuendeleza biashara zao.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza amesema mkutano huo ni mwendelezo wa kukutana na wanachama katika kujenga mtandao wa kibiashara na kubadilishana ujuzi pamoja na kupata elimu za kujijenga kibiashara kutoka Taasisi mbalimbali.
Amesema, Soko linalijengwa Ubungo ni fursa kubwa kwa wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara na TWCC inatekeleza hilo kwa kuendelea kutafuta fursa zaidi za masoko ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda China na bidhaa za China zinazohitajika na wafanyabiashara wa Tanzania.
” Wanawake lazima tunufaike na hii fursa kwa sababu kutakuwa na watu wengi pamoja na fursa za masoko nakupitia mkutano huu tutapata elimu ya namna ya kupata taarifa sahihi za fursa za kibiashara zilizopo kutoka kwa taasisi mbalimbali ikiwemo Mwanga Community Bank, PPRA na NSSF pia tutapata fursa ya kutembelea soko hilo.” Amesema.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wameishukuru TWCC kwa kuendelea kuonesha fursa zenye tija ambazo zitawainua vijana, wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali.