Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Msisima tarafa ya Sasawala Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma,Serikali imeptumia kiasi cha Sh.milioni 470 kujenga baadhi ya majengo katika shule hiyo ili kutoa nafasi kwa watoto wanaomaliza elimu ya msingi kutoka kata ya Msisima kuendelea na sekondari badala ya kwenda kata za jirani.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa kulia,akikagua ubora wa viti vitakavyotumika na wanafunzi katika shule ya Sekondari Msisima wilayani Namtumbo,kushoto Makamu Mkuu wa shule hiyo John Maduka.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Vita Kawawa katikati,akimsikiliza Makamu wa shule ya Sekondari Msisima John Maduka kulia,kuhusu ujenzi wa miundombinu na maendeleo ya shule hiyo,kushoto Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Namtumbo Zuber Lihuwi.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Vita Kawawa,akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Msisima tarafa ya Sasawala iliyopo umbali wa zaidi ya kilometa 280 kutoka Makao makuu ya wilaya Namtumbo ambapo Serikali imetoa Sh.milioni 470 kati ya milioni 600 kujenga shule hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Vita Kawawa,akikagua ubora wa milango katika shule ya Sekondari Msisima wakati wa ziara yake ya kukagua shule za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali na kuzungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali wilayani humo,kushoto Makamu mkuu wa shule hiyo John Maduka.
…………………
Na Mwandishi Maalum,
Namtumbo
MADAKTARI Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili,wanatarajia kuweka kambi ya siku tatu katika kituo cha afya cha Mtakanini kata ya Msindo wilayani Namtumbo,kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa Tezi Dume,Saratani ya matiti na mlango wa kizazi na Sukari.
Mbunge wa Jimbo la namtumbo Vita Kawawa alisema,huduma hizo zitatolewa kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Julai mwaka huu, na ni fursa nyingine kwa wananchi wa Namtumbo kufikiwa na huduma za matibabu za kibingwa katika kipindi cha mwezi mmoja.
“hii ni mara ya pili kupata timu ya Madaktari Bingwa kuja kutoa huduma katika Jimbo letu la Namtumbo,awali kufanyika zoezi la uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kutoka kwa timu ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI)”alisema Kawawa.
Alisema,huduma hizo zitatolewa bure na kuwataka wananchi wa wilaya ya Namtumbo na wilaya nyingine katika mkoa wa Ruvuma,kuchangamkia fursa hiyo kwa kwenda kupata huduma za matibabu kutoka kwa Madaktari hao.
Amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kwenye kambi za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu zilizofanyika kwa muda wa siku saba katika Hospitali ya wilaya Namtumbo,kituo cha Afya Lusewa na Mputa.
Katika hatua nyingine Kawawa,ameipongeza serikaliya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutoa Sh.milioni 470 kati ya Sh.milioni 600 kwa ajili ya kujenga shule ya Sekondari Msisima kata ya Msisima wilayani Namtumbo.
Alisema,shule hiyo imeleta nafuu kwa watoto wanaomaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya Sekondari ambao awali walitembea umbali wa kilometa 30 kwenda kata jirani ya Lusewa kufuata masomo na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kufika kidato cha nne.
Amewaomba wazazi na walezi kuwasimamia na kuwapata mahitaji muhimu watoto wao ili waweze kusoma kwa bidii,kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha na msingi wa maendeleo kwa kuwa wakifanya vizuri kwenye masomo, watakuwa msaada mkubwa kwa familia na Taifa kwa ujumla.
“nawaomba sana watoto wetu someni kwa bidii ili muweze kufanya vizuri kwenye masomo yenu,Serikali imetimiza wajibu wake kuwajengea shule nzuri ili kuwaondolea usumbufu uliokuwepo hapo mwanzo,mumuenzi Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan aliyetoa Sh.milioni 470 kujenga shule na walimu nawaomba wasaidieni hawa vijana wetu waweze kupata elimu bora”alisema Kawawa.
Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Msisima John Maduka,ameiomba Serikali kutoa Sh.milioi 130 zilizobaki ili kukamilisha baadhi ya majengo ya shule ambayo hadi sasa ujenzi wake bado haujakamilika.
Maduka alisema,kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 134 kati ya 400 wanaotakiwa kuwepo kuanzia kidato cha 1 hadi 3,walimu 9 na kuanzishwa kwa shule hiyo ni ukombozi mkubwa kwa watoto wanaomaliza darasa la saba wanaotoka kata ya Msisima Tarafa ya Sasawala.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu Sikuzan Aman alisema,watatumia fursa ya uwepo wa shule karibu na maeneo wanayotoka kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kuishukuru serikali kuwajengea shule hiyo.