Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo vya shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa iliyopo Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, uliogharimu shilingi 61,560,500.
Mkuu wa shule hiyo Samwel Kaitira akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya mwenge wa uhuru, amesema kati ya fedha hizo shilingi milioni 56 ni fedha za Serikali kuu na shilingi milioni 5.6 ni nguvu za wananchi.
Kaitira amesema mradi huo una uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 wa kidato cha tano kwa mkupuo mmoja na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, kuamsha ari ya kusoma kwa bidii na kupunguza mdondoko.
Amesema mradi huo ulianza mwezi Februari mwaka 2024 na mradi umetekelezwa kwa fedha za serikali kwa mwaka 2023/2024 na nguvu za wananchi kupitia mafundi wa ndani.
“Tunapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia fedha zilizotekeleza mradi huu na tunampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, tunasema kazi iendelee,” amesema Kaitira.
Kiongozi wa mbio za mweng wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2024, Godfrey Eliakim Mzava amepongeza mradi huo kwani utaongeza idadi ya vijana nchini kupata elimu ya kidato cha sita.
Mzava amesema mwenge wa uhuru wa uhuru unazindua madarasa hayo kwa lengo husika na kutoa rai kwa vijana watakaoyatumia madarasa hayo wasome kwa bidii ili waelewe masomo na kufaulu.