Na Mwandishi wetu, Mirerani
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Eliakim Mzava ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kituo cha afya Tanzanite kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, utakaogharimu shilingi milioni 500 hadi kukamilika.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani Dkt Namnyaki Lukumay akisoma taarifa ya ujenzi huo amesema kuwa kituo hicho kitakuwa na jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo pacha la wazazi na upasuaji.
Dkt Namnyaki amesema ujenzi wa kituo cha afya Tanzanite ulianza machi 22, mwaka 2024 na kinatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi oktoba 2024.
Amesema lengo ni kutimiza azma ya Serikali ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika kituo cha afya Mirerani na kuzidi kusogeza huduma bora za afya kwa karibu na jamii ya mji mdogo wa Mirerani.
Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi ameishuku serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi milioni 500 za ujenzi wa kituo hicho cha afya Tanzanite.
Salome amesema kituo hicho cha afya pamoja na kuwasaidia wakazi wa kata yake pia kitapunguza msongamano kwenye kituo cha afya kilichopo kata ya Endiamtu.
“Nawapongeza mno viongozi wa kamati ya ujenzi wakiongozwa na Mwenyekiti wao mdau wa maendeleo Taiko Ole Kulunju na katibu wake Charles Nyasuka kwa usimamizi mzuri na wakizalendo,” amesema Salome.
Amesema Taiko na Nyasuka wamekuwa chachu ya maendeleo kwani huwa wanatoa hata fedha zao binafsi mfukoni pindi ujenzi ukikwama ili ueendelee hivyo anawapongeza mno.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2014 Godfrey Eliakim Mzava baada ya kukagua hatua za ujenzi ameridhishwa na kuweka jiwe la msingi na kupanda miti katika eneo la kituo cha afya.
Mzava pamoja na kupongeza ujenzi huo amesisitiza hatua zillizosalia zikamilishwe kwa wakati na ubora ili huduma zianze kutolewa.
“Tunatarajia kituo kitaanza kufanya kazi pindi kikikamilika na jamii ya eneo hili ianze kupata matibabu hapa karibu,” amesema Mzava.
Mwenge wa uhuru mwaka 2024 unaongozwa na kauli mbiu isemayo tunza mazingira na shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ujenzi wa Taifa endelevu.