Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) aliweka mkono kuashiria uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo Julai 20,2024 Mkoani Kigoma. Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura umeanza rasmi leo katika mikoa ya Kigoma, Katavi na tabora na zoezi hilo linafanyika kwa siku saba hadi tarehe 26 Julai, 2024.
hina Sikabwe mkazi wa Mtaa wa Kawawa Kata ya Kipampa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji mkoani Kigoma baada ya kujiandikisha kuwa Mpiga Kura.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) akigusa kishikwambi kuzindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma.
“Nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa zoezi hilo lina lengo la kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Magereza kuweka miundombinu wezeshi ili kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutekeleza wajibu wake wa kuandikisha wafungwa wenye vifungo chini ya miezi sita na mahabusu kwa ufanisi.
“Hii fursa ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuwawezesha magereza kupiga kura ya kuchagua viongozi wanaowataka, hii mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kutoa fursa kwa wafungwa na mahabusu kupiga kura wakiwa magerezani”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia watanzania kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kuwa chaguzi zote zitakuwa huru na Haki.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga amesema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia,Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile Vijana, Wanawake nawatu wenye Ulemavu . Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini”
Naye, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele amesema kuwa Jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar.
“Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka 2019/2020”.
Viongozi na wazee wa kimila nao ni wadau wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hivyo nao walihudhuria.
Viongozi wa vyama vya siasa ni wadau wakuu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, nao waliokuwa ni miongoni mwa walioshiriki katika uzinduzi huo.
Wasanii Peter Msechu, Sande Linex na Dulla Makabila nao walishiriki kwa kutoa burudani kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma waliohudhuria uzinduzi huo wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura mkoani Kigoma.