Mh. Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Dkt Lazaro Komba akiwa katika mkutano wa hadhara katika Kijiji Cha Santamaria
……………..
NA Neema Mtuka ,Kalambo
RUKWA
Mkuu wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Dkt Lazaro Komba amewataka wananchi wilayani humo kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa lengo la kupata viongozi bora na wenye tija katika jamii.
Ameyasema hayo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Santamaria wilayani humo na kusisitiza wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mikoa ya Kigoma Rukwa, Njombe, Songwe na Ruvuma.
Aidha zoezi la Uandikishaji katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linatarajiwa kuanza tarehe 11/10/2024 hadi 20/10/2024 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika tarehe 27/11/2024 katika vijiji 111 vya Jimbo la Kalambo.
Kaimu afisa utumishi wilayani humo Laurent Kaprimpiti amesema serikali imeanza maandalizi ya zoezi la uandikishaji wa kupata vitambulisho vya wapiga kura kwa wananchi waliotimiza umri wa kupiga kura miaka 18.
Hata hivyo zoezi la Uandikishaji kwa ajili ya kuboresha daftari la Kudumu la wapiga Kura katika Uchaguzi mkuu linatarajiwa kuanza tarehe 12/01/2025 hadi 18/01/2025.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi akiwemo Siwema Julius amesema atahakikisha anajiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga kura kwani ni haki yake ya msingi.
Nao viongozi mbalimbali wa dini waliohudhuria mkutano huo wa hadhara wamesema ni haki ya msingi ya kila raia wa tanzania kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.