NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha Elina Mgonja amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha wanaungana kwa pamoja katika kukabiliana na wimbi la vitendo vya utekaji wa watoto.
Mgonja ameyasema hayo wakati akizungumza na wanawake wa UWT katika kata za Mbwawa na Msangani wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuangalia uhai wa chama pamoja na kuhimiza wanawake kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba kumekuwepo na matukio mbali mbali ya baadhi ya watoto kufanyiwa vitendo vya kutekwa na wengine kufanyiwa vitendo vya kulawitiwa.
“Wanawake,wazazi pamoja na walezi mnapaswa kuhakikisha kwamba mnawalinda na kuwatunza watoto wao kwani kuna wimbi kubwa la utekaji kwa watoto kwa hivyo inabidi tuwe makini sana,”alisema Mgonja.
Aidha aliwahimiza wanawake kuhakikisha kwamba wanaungana kwa pamoja katika kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.
Kadhalika aliwakumbusha wanawake kuweka utaratibu wa kuwachunguza kwa kina watoto wao ili kuweza kubaini kama wamefanyiwa vitendo mbali mbali vya ukatili ikiwemo kulawitiwa.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT Kibaha mjini Dkt.Zainabu Gama amewataka wanawake kutokuwa waoga kabisa na kuchukua maamuzi ya kuwa Jasiri.
Naye Diwani wa viti maalumu wa Halmashauri ya mji Kibaha Lidia Mgaya amewaomba wanawake kuwa na umoja na upendo na kuwa mstari wa mbele hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ziara ya Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imelenga kupita katika kata zote za 14 kwa lengo la kuwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi za uongozi.