*Zajadili ushirikiano katika utafutaji, usambazaji wa Gesi Asilia na Mafuta
*Tanzania yaikaribisha Indonesia uendelezaji wa Jotoardhi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na kufanya mazungumzo na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Pahala Mansury ambapo mazungumzo yao yalijikita katika kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika Sekta ya Nishati.
Kikao kati ya viongozi hao kilifanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wataalam kutoka nchini Indonesia.
Katika kikao hicho, nchi hizo mbili zilikubaliana kuongeza ushirikiano kupitia Hati ya Makubalino (MoU) kati ya kampuni ya Pertamina ya Indonesia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
kutokana na mafanikio ambayo tayari yamepatikana ikiwemo kuwajengea uwezo Wataalam kupitia mafunzo ya muda mfupi katika tasnia ya mafuta na gesi.
Aidha, nchi hizo mbili zilijadiliana kuhusu ushirikiano katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi katika vitalu vya nchi kavu na Baharini kwani kwa sasa Wizara kupitia TPDC inatafuta wawekezaji wa kushirikiana nao katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo na Eyasi Wembere.
Pia, Ushirikiano katika shughuli za usambazaji wa Gesi asilia nchini ulijadiliwa katika kikao hicho ambapo
Ilielezwa kuwa, Serikali ya Tanzania inatekeleza miradi ya usambazaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya magari na majumbani hivyo imeiomba Indonesia kuwekeza katika miradi hiyo nchini kupitia kampuni zenye uzoefu wa kazi husika.
Tanzania na Indonesia pia zimejadiliana kuhusu ushirikiano katika utafutaji wa rasilimali za joto ardhi nchini wakati huu ambapo Serikali inaendelea na shughuli za utafutaji wa rasilimali hizo ikiwemo uchimbaji wa visima vya tafiti katika maeneo yenye viashiria vya Jotoardhi mkoani Songwe na Mbeya.
Vilevile, Wizara ya Nishati imeialika Indonesia kushiriki katika Kongamano la Afrika la Jotoardhi linalotegemewa kufanyika nchini hivi karibuni ili kufahamu zaidi fursa katika Sekta.
Ujumbe kutoka Indonesia ulitumia fursa hiyo kuialika Tanzania katika Kongamano la Kibiashara kati ya Indonesia na nchi za Afrika (Indonesia – African Business Forum)
litakalofanyika mwezi Septemba mwaka huu ambalo litahusisha masuala mbalimbali ikiwemo majadiliano katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati.