Na Mwandishi Wetu,WHMTH, Shinyanga
Wakati laini za simu zilizosajiliwa nchi nzima zikifikia milioni 72.4, Mkoa wa Shinyanga pekee, zimesajiliwa laini 1,966,528 ikiwa ni sawa na 2.71% ya laini zote nchini.
Hayo yamebainishwa tarehe 19 Julai, 2014 na Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakili John Daffa wakati akitoa wasilisho la hali ya huduma ya mawasiliano kwa mkoa huo, mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Nape Moses Nnauye (Mb), na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
“Ukuaji wa usajili wa laini za simu umeongezeka kwa asilimia 19.8 kutoka Juni 2022 hadi Machi 2024 ambapo jumla ya laini za simu zilizosajiliwa ni 1,966,528 kutoka line 1,641,547,” amesema Wakili Daffa, katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa.
Amesema, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Shinyanga ina wakazi 2,241,299 na kwa ulinganifu wa idadi ya watu na laini za simu ni sawa na asilimia 87.74%.
Kuhusu hali ya ufikiwaji wa huduma za mawasiliano katika Mkoa, Wakili Daffa amesema, umeimarika kwani wanaopata mawasiliano ya 2G ni 99.5%, 3G ni 99%, 4G ni 96.66% na 5G ni 2.68.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa mawasiliano ya simu na inteneti mkoani Shinyanga, Wakili Daffa amesema, ili huduma ziweze kupatikana ni lazima miundombinu ijengwe na tayari minara 257 imejengwa hadi kufikia mwaka 2024.
Wakili Daffa amesema, TCRA inaimarisha ushirikiano na wadau katika kutatua changamoto hususani usalama wa mitandao inayochangiwa na uelewa mdogo wa watumiaji wa huduma hizo, uhalifu mtandaoni na mawasiliano hafifu kwa baadhi ya vijiji.
Amesema, kwa kutambua kuwa Sekta ya Mawasiliano ni sekta wezeshi inayokuwa kwa kasi na kufungua fursa mbalimbali, usimamizi thabiti unafanyika ili kuongeza mchango wake katika uchumi na maendeleo ya Taifa.