Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Nimewahi kuandika makala siku za nyuma isemayo “Tusaidie kufanikisha kampeni hii ya Fichua.” Katika makala hii nilieleza kampeni iliyozinduliwa Juni 28, 2024 na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) iliyopewa jina la “Fichua-Kuwa Hero wa Madogo” yenye lengo la kuwahamasisha wananchi kuwafichua wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Wanufaika hawa wanaosakwa na bodi ya mikopo ni wale ambao kwanza wameshahitimu masomo yao na pili wana vipato halali vinavyowaingizia fedha yaani waliojiajiri na walioajiriwa na hivyo wana uwezo wa kuanza kulipa fedha walizokopeshwa lakini bado hawajaanza kurejesha mikopo yao. Ieleweke kuwa msingi wa kampeni ya Fichua si kuwafichua wahitimu walionufaika na mikopo ambao hawana kazi au vipato bali ni kwa wahitimu wenye vipato ambao bado hawajaanza kurejesha mikopo, hii ieleweke vizuri.
HESLB imepewa jukumu kubwa la kupokea na kushughulikia maombi ya mikopo kutoka kwa waombaji ili wale wenye sifa za kupata mikopo hiyo waweze kupata na hatimaye kutimiza malengo yao ya kupata elimu ya juu katika taasisi mbalimbali za elimu.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na serikali yetu za kuboresha sekta ya elimu katika ngazi zote yaani kuanzia elimu ya msingi hadi ya juu, kumekuwa na mahitaji makubwa ya mikopo kutoka kwa waombaji. Ongezeko hili la waombaji wengi limesababisha HESLB kushindwa kutoa mikopo kwa waombaji wote, wengi wakipata asilimia kubwa, baadhi hupata asilimia ndogo huku wengine wakikosa kabisa.
Kimsingi, hakuna mwombaji wa mkopo ambaye anatamani kupata mkopo kwa asilimia ndogo, mathalani asilimia 20 au 30 au akose kabisa, ni hitaji la kila mwombaji kupata mkopo kwa asilimia 100, 90, 80 au 70 ili kupata unafuu wa kumudu gharama za elimu ya juu kutokana na waombaji wengi kutoka familia zisizo na uwezo kiuchumi, hivyo kupata kwao mikopo huwapa uhakika na utulivu wa kusoma.
Inapotokea mwombaji akapata asilimia ndogo au akakosa kabisa, husababisha baadhi ya familia kuuza mali kama vile mifugo, mashamba, pikipiki, baiskeli huku wengine huchukua uamuzi wa kuahirisha masomo kabisa. Hii ina maana kuwa wapo baadhi ya vijana ambao ndoto zao za kufika elimu ya juu zimefifia kutokana na kukosa mkopo.
Serikali yetu inatambua vyema hali za kiuchumi za raia wake, na ndiyo maana mwaka 2004 ikaamua kuanzisha HESLB ili isaidie kutoa mkopo huku serikali kuu ikiwajibika kuiwezesha bodi kwa kuipatia raslimali fedha za kuwakopesha waombaji wenye kiu ya kusoma elimu ya juu, huku wanufaika hao wakiwajibika kurejesha mikopo hiyo pindi wanapohitimu masomo yao na kuwa na vipato halali ambavyo ndiyo nyenzo ya kuwawezesha kulipa mikopo hiyo. Tangu HESLB ianzishwe mwaka 2004, wapo wanufaika wengi sana waliopata mkopo.
Pengine ni muhimu kwa wanufaika wa mikopo kulipa mikopo yao sasa na pia wanapaswa kuelewa kuwa wanaopaswa kurejesha mikopo ni wale wenye vipato kwa maana wameajiriwa serikalini au katika sekta binafsi au wamejiajiri wao wenyewe, muhimu wawe na vipato halali. Basi. Mtazamo kuwa mnufaika anapaswa kulipa mkopo wake pale tu anapopata kazi serikalini na kwenye sekta binafsi na si katika shughuli yake binafsi aliyojiajiri kama vile mamalishe, bodaboda, fundi nguo, uashi, ni dhana potofu.
Ndugu msomaji wangu, kwa leo tuishie hapa.
Itaendelea sehemu ya pili. Usikose.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.