Na Neema Mtuka ,Sumbawanga
Vijana wametakiwa kuhakikisha wanaongeza bidii ya kusoma na kujifunza ili kwenda sambamba na kasi ya teknolojia na kwenda sawa na ulimwengu wa sasa wa kidigitali .
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku 3 iliyoifanya mkoani Rukwa ambapo pamoja na mambo mengine ameweka jiwe la msingi katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Mbeya Kampusi ya Rukwa (MUST) .
Rais samia amesema mradi huo utaleta mapinduzi katika elimu ya juu ambapo utawasaidia vijana kupata mafunzo kwa vitendo ambavyo vitawawezesha kujiajiri na kuajiriwa .
Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Mbeya kampusi ya Rukwa Waziri wa elimu sayansi na teknolojia Prof Adolf Mkenda amewataka watumishi wa chuo hicho kusimamia maadili na weledi wa taaluma zao ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kujipambanua kwa vitendo zaidi .
Prof Mkenda amesema chuo hicho kimefungua milango kwa vijana na watapata elimu na mafunzo kwa vitendo wanayo stahili ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ajira.
Sambamba na hilo Prof Mkenda amesema ni muhimu majengo ya chuo hicho yatunzwe vizuri ili na vizazi vijavyo viweze kutumia majengo hayo na kuhakikiksha miundo mbinu yote inayozunguka chuo hicho inatunzwa kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Zaidi ya shilingi Bill 15 zimetumika katika ujenzi wa chuo hicho ambapo ujenzi wake bado unaendelea na utakamilika mwezi Desemba mwaka huu .
Chuo kikuu cha Sayansi naTeknolojia cha Mbeya Kampusi ya Rukwa kinapokea pia wanafunzi kutoka katika nchi mbalimbali ikiwemo nchi jirani ya Zambia Rwanda Burundi Kenya Uganda na Botswana.
Rais Dkt. Samia amemaliza ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani rukwa na kurejea katika majukumu mengine ya ujenzi wa Taifa ambapo ameacha neema na faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa huo.