Muonekano wa barabara zilizojengwa kwa teknolojia ya kisasa ya “Ecoroads’ katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila ( wa kwanza kulia ) wakiangalia barabara zilizojenmgwa na TARURA wilayani Chamwino. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff na kushoto mwenye shati la pinki ni meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma Mhandisi Edward Lemelo.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila (kushoto) wakijadiliana na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati wa kukagua barabara zilizojengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa wilayani Chamwino
Ukaguzi wa barabara zenye urefu wa Km. 6.95 zilizojengwa kwa teknolojia ya kisasa wilayani Chamwino ambapo tathimini yake inaonesha mafanikio makubwa na ubora baada ya miezi sita kupita tangu kukamilika na kutumika.
…………
Na. Catherine Sungura,CHAMWINO
Teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa barabara kwa kuboresha udongo kabla ya kuweka lami juu ijulikanayo kama ‘Ecoroads’ imeonesha matumaini katika miezi sita ya majaribio.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila mara baada ya kutembelea Barabara zilizojengwa na teknolojia hiyo yenye urefu wa Km. 6.95 wilayani Chamwino.
Mhandisi Mativila amesema kwamba lengo kubwa la kutembelea barabara hizo ni kujionea mafanikio ya matumizi ya teknolojia hiyo ambayo pia inajaribiwa katika wilaya mbalimbali nchini na inatekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
“Lengo la kuja kutembelea barabara hii hapa Chamwino ni kuangalia mafanikio ya matumizi ya teknolojia hii ya kisasa ya kuboresha udongo kabla hatujaweka lami juu inayotekelezwa na TARURA”.
Amesema teknolojia hiyo pia inafanyiwa majaribio huko Mufindi, Rufiji na maeneo mengine ili kuweza kuitumia sehemu nyingine ambapo inaweza kupunguza gharama na muda wa ujenzi wa barabara.
“Barabara hii iliyojengwa inaonekana ni imara na pia sehemu nyingine ya Km. 1.3 haijawekwa lami ila udongo uliokuwa pale umechanganywa na kemikali ambayo tunaendelea kufanyia majaribio tuweze kuona mafanikio yake”.Aliongeza
“Tunafanya hivyo ili kuona kabla haujafunika na tabaka la juu inayozuia maji na vitu vingine je! inaweza kudumu kwa muda mrefu na tayari imeshakaa kwa muda wa miezi sita na tumekuta bado ipo imara kwahiyo inatuonesha hii kemikali inayotumika inahimili na malighafi ni nzuri lakini bado tunaendelea kuiangalia ili tukiona imefanikiwa itatumika kwa kiwango kikubwa kwenye ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA”.
Wakati huo huo , Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema teknolojia hiyo wilayani Chamwino ni sehemu ya majaribio na tayari wameshafanya katika maeneo mbalimbali ikiwemo barabara ya Ilazo-Dodoma (Km. 1) Sawaka-Mkonge-Iyegeya-Lulanda-Mufindi (KM. 10.4) na Utete-Kingupila-Rufiji (Km. 32).
“Tangu ujenzi kukamilika hapa Chamwino tayari imeshapita zaidi ya miezi sita lakini bado barabara zina hali nzuri hivyo sasa hivi tunaendelea na tathimini ya mafanikio ya hii teknolojia yenyewe ili hapo baadae tuje tuishauri serikali kama teknolojia hiyo iendelee kutumika katika ujenzi na matengenezo ya barabara zetu”.
Amesema lengo la kuwa na hizo teknolojia ni kupunguza gharama, kuwa na muda mfupi wakati wa ujenzi pamoja na utunzaji wa mazingira.
Mhandisi Seff ameongeza kusema kwamba licha ya gharama kuwa ndogo lakini bado kuna utofauti ukilinganisha na ujenzi wa kawaida ambapo faida ya teknolojia hiyo unaiona moja kwa moja katika muda wa utekelezaji kuwa mfupi akitolea mfano barabara hiyo ya Chamwino ambayo mkataba wake ulikuwa wa mwaka mmoja ila wameweza kujenga na kukamilisha ndani ya miezi sita.
Naye, Fundi wa magari kutoka mtaa wa Mshikamamo Bw. Songo Yusufu amesema barabara hizo za sasa ni bora kuliko za mwanzo ambapo ujenzi wa barabara hizo zimerahisisha kufikiwa na wateja wake kwa urahisi kwani awali barabara ilikuwa na vumbi pamoja na mashimo mengi.
Amesema anamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea barabara hizo kwani mji umeweza kukuwa na huduma muhimu za msingi wameweza kupatiwa ikiwemo maji na hivyo Chamwino kuwa ya kisasa.