Na Majid Abdulkarim, RUKWA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya nchini kuhamasisha suala la bima ya afya kwa wote ili watanzania wawe na uhakika wa huduma ya matibabu muda wote.
Akihitimisha ziara yake ya siku tatu Mkoani Rukwa, leo Julai 17, Rais Samia amesema suala la bima ya afya kwa wote ni muhimu ambapo kila Mtanzania anatakiwa kuwa na bima hivyo viongozi wa Mikoa na Wilaya ni lazima waweze kuwaelimisja kila mmoja awe na bima yake.
“Niwaombe sana viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya pale watakapokuwa tayari, nawaomba wananchi kwa upande wenu kila mmoja ahakikishe anakuwa na bima ya afya ambayo unainunua mara moja tu kwa mwaka na unatibiwa mwaka mzima.
Amewataka wakazi wa mkoa wa Rukwa pindi watakapovuna mazao yao wahakikishe wanakuwa na bima ili waweze kupatiwa matibabu pindi wapatapo changamoto ya afya.
“Unapovuna Mahindi ukirudi NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) toa kiwango kilichowekwa nunua bima yako na mama na watoto mwaka mzima mtatibiwa kwa bima hiyo.Usiponunua bima maradhi hayana salamu yanaweza yakakutokea wakati huna fedha.
“Tunakwenda Hospitali ukitaka kuchukuliwa vipimo unaambiwa nenda kalipe kwenye vipimo huna fedha unarudi nyumbani unakaa na maradhi yako, lakini ukiwa na bima yako vipimo vyote vinabebwa na bima yako ya afya,”amesema Rais Samia
Amesema kwa upande wa Serikali kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge walianzisha vyanzo vichache ambavyo vitawapa fedha kwa ajili ya makundi yasiyonauwezo ambayo ni kina mama wajawazito, watoto na wazee wasio na uwezo.