Na Sabiha Khamis – Maelezo
Wizara ya Maji, Nishati na madini imetia saini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya umeme na Kampuni ya umeme, Zhonglian Technology (ZTT) na SIEYUAN kutoka China ili kuondoa tatizo la umeme Nchini.
Akizungumza katika halfa ya utiaji saini mikataba hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Mhe. Shaib Hassan Kaduara, amesema utekelezaji wa mradi huo utafungua njia tofauti za kiuchumi na kusaidia kuinua uchumi wa nchi hasa katika sekta ya utalii.
“Uchumi wa nchi ili uweze kukua na kuwa endelevu lazima kuwepo na upatikanaji wa miundombinu ya umeme iliyobora” amesema Waziri Kaduara.
Aidha amewaomba wakandarasi hao kutekeleza mradi huo kwa wakati ili kutatua changamoto za umeme mdogo kwa wananchi wa Zanzibar pamoja na kuwataka wafanyakazi wa shirika la umeme kutoa mashirikiano ili ufanikisha mradi huo kwa wakati uliopangwa .
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph J. Kilangi amesema lengo la mradi huo ni kutatua changamoto zilizopo ikiwemo umeme mdogo kwa baadhi ya maeneo pamoja na upotevu wa umeme .
Amefahamisha kuwa utekelezwaji wa mradi huo wa laini za umeme ya 152 Kilo Volti ambayo itajengwa kwa urefu wa kilomita 99.9 sawa na asilimia 100 pamoja na vituo vya kupoozea umeme ambavyo vitakuepo katika maeneo ya Makunduchi na Matemwe.
Aidha ameelezea kuwa umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na husaidia kukuza utalii ambao ndio chanzo kikuu cha pato la taifa
“Katika hili tunakwenda kufungua njia za utalii kwa Mkoa wa Kaskazini na Kusini pamoja na kupunguza upotevu wa umeme na kuweka nguzo za umeme kwa wanaohitaji” amesema Katibu Kilangi.
Sambamba na hayo amewataka wananchi ambao wameshalipwa fidia zao kuondoka katika maeneo hayo na ambao hawajapatiwa fidia utaratibu unaendelea na hivi karibuni watapatiwa ili kupisha ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu Shirika la umeme Zanzibar Haji Juma Haji amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya umeme ambapo ukikamilika na kuwa wa uhakika utavutia wawekezaji wa viwanda vya kati na kusaidia katika kuongeza ajira Nchini.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo kutawashajihisha wananchi kutumia nishati ya umeme katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia na kuokoa sehemu kubwa ya mazingira.
Amesema Shirika limejipanga kukamisha mradi huo kwa wakati uliopangwa na kuleta tija kwa watumiaji jambo ambalo litaleta mafanikio kama yalivyokusudiwa na Serikali.
Mikataba miwili imesainiwa na Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Haji Juma Haji na Meneja Idara ya Uhandisi Miao Xiaonan kutoka Kampuni ya ZTT pamoja na Mwakilishi Mkuu wa Afrika Kusini Yan Yun kutoka Kampuni ya Sieyuan Electric kutoka China.