Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua leo tarehe 16 Julai 2024 vihenge na maghala ya kisasa ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), katika eneo la Kanondo, Mkoani Rukwa.
Wakati wa mazungumzo yake na wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Rais Dkt . Samia ameelekeza kuwa mbolea za ruzuku ziendelee kuwepo na kusisitiza mahindi yanunuliwe kutoka kwa wakulima wa vijijini kwa gharama ya shilingi 600 kwa kilo; na mjini shilingi 650 kwa kilo.
Aidha, alitilia mkazo kwa wananchi kutosafirisha mahindi nje ya nchi bila vibali vya Wizara ya Kilimo; na taratibu nyingine zinazotakiwa kwa kuwa zinaathiri uchumi na soko la kibiashara. Kuhusu mizani ya kidigitali, Mhe. Rais Dkt. Samia alielekeza ziongezwe kwa wingi katika vituo vya Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) ili kurahisisha huduma kwa wakulima kwa kupata haki stahiki ya uzito wa mazao yao.
Viongozi mbalimbali walishiriki katika uzinduzi huo, akiwemo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo, Dkt. Andrew Kolimba, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Bodi na Menejimenti ya NFRA; pamoja na mamia ya wananchi wa mkoa wa Rukwa.
Mradi huo utaiwezesha NFRA kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka za aina tofauti kama vile mahindi, mtama na mpunga katika Mkoa wa Rukwa kutoka tani 33,500 hadi tani 58,500; kwa maana ya ongezeko la vihenge tani 20,000 na maghala tani 5,000.
Maghala hayo ya kisasa yana mfumo mzuri wa kupitisha hewa ambao pia unaoruhusu ufanisi katika uhudumiaji mazao (improved ventilation sytem and improved logistical system); ikiwa ni pamoja na utumiaji wa zana mbalimbali za kazi (matrekta, mizani, elevators).
Mradi huo ulianza mwezi Julai 2019 na umegharimu Dola za Marekani milioni 6,019,000 sawa na takribani shilingi bilioni 14. NFRA inaendelea kujipanga kuongeza uwezo wa teknolojia ya vihenge na maghala ili kuendana na uzalishaji wa chakula hapa nchini.