Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko, eleo akiwasilisha mada ya ushiriki wa vyombo vya habari katika kupiga vita mauaji ya alibino jijini Mwanza.
Katibu Tawala Msaidizi ,Utawala na Rasimalimali Watu Mkoa wa Mwanza, Daniel Machunda, akifungua mdahalo wa kupinga mauaji ya watu wenye ualbino leo.
Ofisa Polisi Jamii, Denis Kunyanja, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,leo akieleza majukumu ya jeshi hilo katika kuwalinda watu wenye ualbino wakati wa mdahalo.
Mchungaji Dk.Jacob Mustash, akizungumza katika mdahalo wa kupinga mauaji ya albino uliondaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na TAS.
……..
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
WANASIASA,waganga wa tiba asili na tiba mbadala,wachimbaji madini na wavuvi wanadaiwa kuchochea mauaji ya watu wenye ualbino ili kupata vyeo na utajiri.
Wamesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani,yameanza kuibuka mauaji ya watu wenye ualbino na kuzua hofu kwa kundi hilo likihofia usalama wao.
Mwenyekiti wa TAS Mkoa wa Mwanza, Stallone Makoye ameeleza kuwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika maka huu au wakisikia tukio limempata mwenzao wanajikuta wakiishi kwa hofu ambapo tangu mwaka 2020 matukio manne ya ukatili waliofanyiwa wenye ualbino mmoja alipoteza maisha.
“Matukio haya yamerudi tena,ripoti ya 2006 hadi 2015 watu wenye ualbino 75 wameshapoteza maisha na matukio sasa yana tokea mfululizo,mfano mtoto mdogo Asimwe aliyekuwa na ualbino aliuawa huko Kagera,”amesema.
“Suala hili linawahusisha wanasiasa na waganga wa jadi, ambao ni watuhumiwa wa kwanza.Kwa nini serikali inawapa leseni waendelee kutoa huduma,kusema serikali inatulinda mnataka kuturudisha kuishi kambini ama mtaani tukipita tuitwe deal,hatutaki kurudi huko sheria isimamiwe mtu akikamatwa anahusika akitiwa hatiani anyongwe,”amesema mdau mmoja akiomba hifadhi ya jina.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wavuvi Kanda ya Ziwa,Bakari Kadabi amesema tunapolekea kwenye uchaguzi tukae na wanasiasa tuwambie wanatuumiza,ndiyo maana tunapata baadhi ya wabunge wasiotetea wananchi.
“Tunazungumza uhai wa watu wenye ualbino,tunahafamu sababu za kuuawa kwao na nani wanatajwa kuhusika,wanatafutwa wakati gani,bila kuwataja wahusika mauaji yataendelea kwa sababu wavuvi na wachimba madini wanavua na kuchimba mwaka mzima bila mauaji kutokea,hivyo tuweke mikakati na viongozi wa serikali”amesema.
Mwenyekiti wa TAS Wilaya ya Ukerewe,Charles Kalilo amesema; “Tusizunguke, wanasiasa wanahusika katika kadhia hii na ikitokea mwanasiasa akakamatwa ahojiwe ili mnyororo huo ufahamike kisha wafutwe (wapigwe risasi),hilo likifanyika wataogopa,lakini kuendelea na siasa tutakwisha.”
Hata hivyo mmoja wa viongozi wa waganga wa tiba asili na tiba mbadala mkoani humu (jina linahifadhiwa),amesema kutumia viungo vya binadamu (albino) kupata utajiri ama mvuto kwa watu utamaduni huo Tanzania haukuwepo,umetoka nchi za magharibi mwa Afrika.
“Waganag tunashindwa kuwaeleza watuhali halisi,kutumia viungo vya binadamu mwenye ualbino kupata utajiri utamaduni huo haukuwepo na tunahafamu utajiri mtu anaurithi kwa babu wala si kiungo cha binadamu,”amesema.
Mtalaamu huyo wa tiba asili ameeleza imani potofu hiyo imewakumba wachimba madini wakiamini kutumia viungo vya albino watapata madini,wanasiasa wakivitumia wanakuwa na na mvuto kwa watu hata baadhi ya viongozi wa makanisa wana imani hiyo potofu.
Awali akisoma risala ya TAS mkoani Mwanza,Mashaka Tuju,amesema tangu mwaka 2006 hadi 2024 watu wenye ualbino 20 wameuawa na kuufanya mkoa kinara wa mauaji ya watu wenye ualbino,bado mauaji hayo yameendelea kuwepo hasa uchaguzi unapokaribia.
“Watu wenye ualbino wanakumbwa na manyanyaso na ukatili,wanauawa kwa imani potofu,wanateswa, wananyanyswa,wana uoni hafifu na wanakosa mafuta maalumu ya kulinda ngozi pamoja na elimu ndogo kwa jamii kuhusu ualbino,”amesema Tuju.
Amesema mauaji ya albino yana mkono wa wanasiasa na yanaapuuzwa kwa sababu ndani na nyuma ya mauaji hayo kuna wanasiasa wakubwa,hivyo wamechoka Tanzania inayoitwa kisiwa kisiwa cha amani isipobadilika itavurugika.
Akifungua mdahalo huo Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu),Mkoa wa Mwanza,Daniel Machunda amesema watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino watachukuliwa hatua za kisheria na kuwafikisha mahakamani.
Amesema kongamano la kupinga mauaji ya watu walio kwenye kundi hilo siku za usoni yameibuka matukio ya kuhatarisha usalama wao maeneo mbalimbali,mikakati imewekwa na serikali ya mkoa yanayolenga mapambano dhidi ya vikongwe na wenye ualbino kuhakikisha kila mwananchi anapata ustawi wake binafsi na jamii kwa ujumla.
“Mauaji hayo yatia aibu na kutushushia thamani,kama jamii tuseme imetosha na tusikubali vitendo hivi viendelee,kila mmoja akatae kutapeliwa na waganga wapiga lamli chonganishi wanaoleta imani potofu katika jamii,”amesema Machunda na kusisitiza ni mambo ya ovyo yasiyotakiwana yasiyokubalika,ni vitendo haramu na viovu katika jamii mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Ofisa Polisi Jamii mkoani Mwanza,Denis Kunyanja,akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC),Wilbrod Mutafungwa,amesema tabia ya jamii kuficha wahalifu ni mabaya isiyovumilika hivyo wanafurahi kuwa sehemu ya mdahalo huo kwa sababu polisi wanalo jukumu la kuwalinda watu wenye ualbino.