Meli ya Hospitali kutoka Jeshi la Ukombozi wa watu wa China ikiwa nchini Tanzania kwa ajili ya kutoa matibabu ya kitabibu bure kwa watanzania ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila (wa kwanza kushoto) akiwa Mkuu wa Huduma za Tiba Jeshini Meja Jenerali Amiri Mwami (katikati) pamoja na Maskali wa Jeshi la Ukombozi wa watu wa China katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya matibabu ya kitabibu yanayotolewa bure na JWTZ kwa kushirikiana Jeshi la China, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China.
Mkuu wa Huduma za Tiba Jeshini Meja Jenerali Amiri Mwami akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa matibabu ya kitabibu yanayotolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa matibabu ya kitabibu yanayotolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Jeshi la Ukombozi wa watu wa China, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika uzinduzi wa matibabu ya kitabibu yanayotolewa bure na JWTZ kwa kushirikiana na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la JWTZ tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China, uzinduzi huo umefanyika leo Julai 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam. (Picha Noel Rukanuga)
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Zaidi ya watu 350 wakiwemo Madaktari Bigwa 140 kutoka Jeshi la Ukombozi wa watu wa China wamewasili nchini wakiwa na Meli kubwa ya hospitali yenye vifaa vyote vya matibabu ya kitabibu wakiwa na lengo la kutoa matibabu bure kwa watanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la JWTZ tangu kuanzishwa kwake pamoja na ushirikiano na Jeshi la China.
Akizungumza leo Julai 16, 2024 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila, amesema kuwa ujio wa ugeni huo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na China.
Mhe. Chalamila amesema kuwa meli hiyo imekuja na vifaa vyote vya hospitali kwa ajili kutibu magonjwa ya ndani, magonjwa ya wakina mama pamoja na watoto.
“Huduma za kitabibu zinazotarajiwa kutolewa kuanzia Julai 18 – 24, 2024 katika vipimo, tiba za kawaida, upasuaji wa kawaida, magonjwa ya kinamama, mifupa, njia ya mkojo, macho, pua, koo, meno, moyo, utumbo pamoja na ngozi zilizoungua na moto” amesema Mhe. Chalamila.
Mhe. Chalamila amesema kuwa matibabu hayo yatatolewa kwa ushirikiano na wataalamu wa afya wa JWTZ, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Tumbi, Amana, Temeke, Mwananyamala, Jakaya Kikwete pamoja na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China.
Ameeleza kuwa huduma za kitabibu zinatarajiwa kuanza kutolewa Julai 18 – 23, 2024 , huku akibainisha kuwa kwa siku moja wanatarajia kutoa huduma kwa watu 600.
“Julai 18, 2024 watakuwa katika hosptali ya Lugalo na Kunduchi, Julia 19, 2024 watakuwa Amana na Bunju, Julia 20, 2024 watakwenda Mwananyamala na Temeke, pia matibabu yataendelea hapa bandarini ndani ya meli hii ambayo ni hospitali” amesema Mhe. Chalamila.
Mkuu wa Huduma za Tiba Jeshini Meja Jenerali Amiri Mwami, amesema kuwa ujio wa meli kubwa kutoka Jeshi la China ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na urafiki uliopo wa Jeshi la Ukombozi watu wa China.
Meja Jenerali Mwami amesema kuwa meli hiyo ni kubwa yenye vifaa vyote vya matibabu katika sekta ya afya ambayo imekusudia kutoa huduma ya matibabu ya afya bure kwa watanzania katika kipindi cha wiki moja.
“Kwa kipindi cha wiki moja madaktari bigwa kutoka China watakaa nchini na watajumuika na madaktari bigwa kutoka hospitali zetu kubwa ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mloganzila, Jakaya Kikwete pamoja na Taasisi ya Mifupa kwa ajili ya kufanya kazi pamoja na kubadilishana uzoefu” amesema Meja Jenerali Mwami.
Amefafanua kuwa pia kutakuwa na madaktari wa kawaida kwa ajili ya kutoa matibabu ya msingi ambao watakuwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mbagala Zakhem, Bunju Shule pamoja na Kunduchi, huku akieleza kuwa baada ya saa za kazi madaktari pamoja na wauguzi watashiriki michezo mbalimbali.