Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Mchechu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Hyyat Regence jijini Dar es Salaam leo Julai 15, 2024.
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Thobias Makoba akifafanua baadhi ya mambo wakati wa mkutano katika ya Msajili wa Hazina na Wahariri wa vyombo vya habari.
……………….
Na Grace Semfuko, Maelezo
Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Mchechu amesema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao cha pili cha Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kinachotarajiwa kufanyika Jijini Arusha mwishoni mwa mwezi Agosti ni pamoja na taasisi hizo kuwekeza nje ya Tanzania.
Amesema mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye wakati akifungua kikao chao cha kwanza, aliwaagiza kuanza kuangalia fursa za uwekezaji wa mashirika hayo ya serikali nje ya Tanzania.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari Jijini Dar es salaam, Bw. Mchechu amesema taasisi na mashirika ya umma zinapaswa kuzitazama biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania kwa namna nyingi ikiwepo kufanya uwekezaji katika nchi hizo.
“Kaulimbimu ya kikao hiki itakuwa ni “Mikakati ya Taasisi za Umma kuwekeza nje ya Tanzania”, hii ni changamoto ambayo Mhe Rais alitupatia aliupotufungulia kikao chetu cha kwanza, lakini ni muhimu sana kwa mashirika yetu kujiuliza wanaanza kuzitazama biashara zetu nje ya Tanzania na kuitazama biashara nje ya mipaka ya Tanzania kuna namna nyingi, kuna namna ya kufanya uwekezaji katika hizo nchi na kuna manna biashara yako inaenda kuzigusa hizo nchi” amesema Bw. Mchechu.
Amesema Serikali imekuwa na mikakati ya kisekta, ambapo kuna sekta ambazo inatamani zikimbie ziende nje ya nchi moja kwa moja, huku akitolea mfano sekta ya mabenki ambayo kwa hapa Tanzania, kuna baadhi ya nchi zimewekeza, hivyo ipo haja kwa Tanzania pia kuvuka mipaka ya nchi kwenda kuwekeza nje.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba, amesema mashirika ya umma yana uwekezaji mkubwa wa watanzania na kwamba yamegusa sekta zote ambapo ili kuyasaidia yakue, ni muhimu taarifa zitolewe kupitia vyombo vya habari.
“Mashirika haya ya Umma ni uwekezaji mkubwa wa watanzania , lakini mashirika haya ya umma na taasisi zimegusa sekta zote, na yote yapo chini ya ofisi ya msajili wa hazina, ili kukuza mashirika haya na kuyasaidia yakue ni sehemu ya wajibu wetu, na namna pekee ya kuyakuza ni lazima tupitie kwa wanahabari, tunathamini sana uwepo wenu na hii inamaanisha kwamba tupo katika njia sahihi ya kuboresha tasnia ya habari na katika kuuhabarisha umma wa watanzania” amesema Bw. Makoba.