Mchambuzi na Mtaalamu wa Mifumo ya Malipo kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Octallion Urasa akielezea mifumo ya malipo ya fedha BoT.
……………..
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka watanzania kutumia mifumo ya malipo ya fedha ambayo ni salama na uhakika jambo ambalo litaleta tija katika masuala ya maendeleo.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu ya masuala ya malipo ya fedha, Mchambuzi na Mtaalamu wa Mifumo ya Malipo kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Octallion Urasa, amesema kuwa ni vizuri watanzania wakafata utaratibu ambao ni salama katika malipo.
Amesema kuwa BoT wanayo mifumo ambayo imewaunganisha na wadau wa sekta ya fedha ikiwemo taasisi za fedha pamoja na mitandao ya simu kulingana na malengo.
Ameitaja baadhi ya mifumo kuwa ni mfumo wa TISS ambao una unganisha taasisi za kibenki kwa ajili ya malipo makubwa kuanzia milioni 20 ambao unatumika kwa ajili ya malipo ya serikali hasa wateja wanapolipa huduma za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema kuwa pia kuna mfumo wa TIPS ambao huwaunganisha watoa huduma wote wa mifumo ya malipo ya rejareja kupitia simu za mkononi , benki au “QR” kufanya malipo madogo madogo yasiyokuwa na haraka ambayo ni chini ya shilingi milioni 20.
“Mfumo huu unatumika katika kulipa misharaha, kulipa kupitia hundi kutoka Benki moja kwenda nyengine” amesema
Ameongeza kuwa pia kuna mfumo Jumuishi wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara East Africa EAPS ambao unawezesha kutuma fedha na kupokea katika nchi za ukanda huo.
Ameeleza kuwa mfumo mpya (Mobile Payments) ambao ulianza mwaka 2021 huu umeuganisha kampuni za simu pamoja na Benki.
“Mfumo huu unatumika kuhamisha fedha kutoka benki kwenda katika simu au kutoka katika simu kwenda benki” amesema