Adeladius Makwega-MWANZA.
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza Julai 14, 2024 limesema kuwa kila Mkristo mwenye Ndoa Takatifu anawajibu wa kutembea kifua mbele, huku baba, mama na watoto wakiishi kwa Upendo wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Haya yamesemwa katika dominika ya 15 ya mwaka B wa Kanisa na Padri Andrea Massawe katika Kanisa la Bikira Maria Malikia wa Wamisionari-Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza ambapo Padri Massawe aliongoza misa ya Kipaimara kwa niaba ya Askofu Mkuu Renatus Nkwande ambapo walei kadhaa walipata sakrameti hiyo.
Akitoa kipaimara hicho katika Parokia ya Malya yenye vigango 18 Padri Massawe alisema, Parokia ya Malya ni kubwa,yenye waamini wakarimu hivyo wajibu kueneza Injili ni kila mmoja wetu na hata hao wanaopata Kipaimara.
Akiweka msisitizo wa maisha ya ndoa Padri Massawe alisema,
“Wengine wana ndoa lakini kila mmoja anatoka nyumbani kivyake, kwanini unakuja kusali kivyako? Mnatakiwa hata kukaa pamoja mke na mume hapa kanisani, kama mumeo amesahau kukupa sadaka unamkumbusha, Padri akihubiri suala la baba na mama kuheshimu ndoa uko jirani na mke/mume wako hapo hapo u nachomekea kwa kumfinya na kumkanyaga miguun kukumbusha wajibu wake.”
Akiendelea kuhubiri Padri Massawe aliuliza maswali kadhaa kwa waamini wake.
Wangapi hapa hamna ndoa lakini mnaishi pamoja? Hapo alijitokeza muumini mmoja tu.Huku akielekezwa afunge ndoa mara moja. Likaulizwa swali lingine, wenye n doa hapa kanisani ambao mume na mke wapo, wanyooshe mikono, mikono mitatu ilinyanyuka , miwili katika kwaya na mmoja kutoka kwa waamini.
“Nyinyi wenye ndoa ambao mnaimba kwaya siwezi kusema leo hii mkae benchi moja maana kila mmoja anaimba sauti yake, lakini wanakwaya mbona mnaoana wenyewe kwa wenyewe?Wewe mzee na mama kutoka kwa waamini ebu kaeni pamoja sasa hivi.”
Mama aliyependeza Kanisa alimfuata mumewe na kukaa naye pamoja, huku waamini wakifurahia kitendo hicho.
Kwa hakika kitendo hicho kiliwafurahisha mno waamini wengi na kiliwakumbusha umuhimu wa kufunga ndoa.