Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
Nikukaribishe mpendwa msomaji wangu kuendelea na sehemu ya pili ya makala yetu isemayo “Tusaidie kufanikisha kampeni hii ya Fichua.” Katika sehemu ya kwanza ya makala yetu nilieleza namna ambayo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilivyo na jukumu la kupokea na kuchakata maombi ya waombaji wa mikopo ili wale wenye vigezo vya kupata mkopo waweze kupata na hatimaye wapate elimu vyuoni.
Pia nilieleza namna ambavyo wanufaika wa mikopo walivyo na wajibu wa kulipa mikopo yao baada ya kuhitimu masomo yao hasa baada ya kuwa na shughuli za kuwaingizia vipato yaani kuajiriwa au kujiajiri. Ulipaji wa mikopo unaiwezesha HESLB kuwa na uwezo wa kukopesha waombaji wengi zaidi, hivyo ni muhimu kwa wanufaika wake kulipa mikopo hiyo kwa hiari.
HESLB imebaini baadhi ya wahitimu ambao ni wanufaika wa mikopo wana vipato halali lakini hawataki kulipa mikopo yao, ndiyo maana ikaja na kampeni ya “Fichua-Kuwa Hero wa Madogo’” ili kuwafichua wadaiwa sugu ambao wana vipato lakini hawajaanza kulipa mikopo iliyotumika kuwasomesha katika vyuo mbalimbali, jambo hili limesababisha baadhi ya waombaji kukosa mikopo. Sasa endelea katika sehemu ya pili ya makala yetu:
BUSARA NI KUJIFICHUA MWENYEWE.
Pamoja na kwamba HESLB imeanzisha kampeni hii nzuri, lakini pia kwa kutambua umuhimu wa kurejesha mikopo hii kwa manufaa ya wengine kupata elimu na kutanua wigo wa wanufaika wa elimu ya juu, ni vyema mnufaika yeye mwenyewe akajifichua kwa kuwasiliana na bodi moja kwa moja ili kuweka utaratibu wa kulipa mkopo wake kupitia namba maalum ya malipo (control number) hasa kwa wale waliojiajiri wenyewe.
Kujifichua ni hatua nzuri kwa kuzingatia kuwa waombaji wengi wa mikopo wanatoka familia maskini ambazo haziwezi kumudu gharama za chuo, kwa hiyo kujifichua ni hatua mojawapo ya kutambua umuhimu wa kuwezesha wengine kupata fursa ya kusoma hasa wale wanafunzi wanaotoka familia maskini kupitia marejesho ya mikopo yao.
WAAJIRI FICHUENI WANUFAIKA WA MIKOPO.
Waajiri ni wadau muhimu mno katika kuwafichua wanufaika wa mikopo pindi wanufaika hao wanapopata kazi katika ofisi zao. Kwa upande wa waajiri wa serikali, imekuwa rahisi sana kuwapata wanufaika na mikopo kutokana na mifumo iliyopo sasa na ndiyo maana mwajiriwa mpya wa sekta ya umma anapoanza kazi kama alinufaika na mkopo basi anaanza kulipa deni lake moja kwa moja katika mshahara wake wa kwanza au wa pili tangu aajiriwe.
Changamoto ipo kwa baadhi ya waajiri wa sekta binafsi ambao baadhi yao wamekuwa wakificha au kuchelewa kutuma taarifa za wafanyakazi wao ambao baadhi yao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Kwa hiyo, kupitia kampeni ya Fichua, waajiri wote wa sekta binafsi na umma watoe taarifa sahihi za waajiriwa wao ili serikali kupitia HESLB iweze kukusanya fedha nyingi zaidi ili vijana wengi zaidi wapate mikopo ya kugharamia elimu ya juu.
Kwa hakika, wadau wote yaani wananchi na waajiri tukishikamana pamoja na kutoa taarifa za wanufaika wa mikopo wenye vipato halali, makusanyo yataongezeka maradufu na hivyo kuongeza fursa ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi pengine hata kufikia hatua ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya cheti katika programu mbalimbali. Muhimu zaidi ni kwa wanufaika wenyewe kujifichua kabla ya kufichuliwa na wengine.
Labda niwafahamishe wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu ni kwamba, kulipa mkopo si mpaka uwe umeajiriwa serikalini au katika sekta binafsi yaani ofisini. Mnufaika anaweza kuanza kulipa kidogo kidogo mkopo wake hata kupitia ajira binafsi aliyonayo, mathalani, ajira kwenye kilimo, ufugaji, bodaboda, mamalishe, fundi simu, ujenzi, magari na shughuli kadha wa kadha.
Ikumbukwe kuwa kampeni ya Fichua ni maalumu kwa wanufaika ambao wameshahitimu masomo yao na wana kazi za kuwaingizia kipato lakini bado hawajaanza kulipa mikopo hiyo. “Lengo ni kufichua wadaiwa sugu ambao wana vipato, lakini wako mitaani wanaendelea na shughuli zao na hawashtuki kulipa madeni,” amesisitiza Dk. Kiwia. Ewe mnufaika, lipa deni lako ili kutoa fursa kwa vijana wengi wa Tanzania kupata fursa ya kusoma elimu ya juu ili nao wachangie katika maendeleo ya Tanzania.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462