Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa Vihenge na Maghala ya Kisasa ya kuhifadhia nafaka ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Zoezi hili limefanyika leo tarehe 14 Julai 2024, Mkoani Katavi katika ofisi za NFRA Kanda ya Mpanda -Katavi.
………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuboresha zaidi teknolojia ya uhifadhi, na kujenga maghala zaidi ili kuongeza uwezo wa kuhifashi hadi kufikia tani milioni 3 mwaka 2030.
Amesema Serikali itahakikisha inaiwezesha zaidi NFRA kufikia malengo hayo ili nchi iweze kujitosheleza kwa mahitaji ya chakuka
Rais Dkt. Samia amesema hayo wakati akizindua vihenge, maghala ya kisasa na msimu wa ununuzi wa nafaka wa mwaka 2024/2025 katika Mkoa wa Katavi leo tarehe 14 Julai 2024.
Mhe. Rais wakati wa uzinduzi alisisitiza kuwa maghala haya ni kiashiria tosha kuwa kilimo cha sasa kinahitaji kubadilika na kuwa kilimo cha biashara badala ya mazao ya chakula pekee. Aidha, alihimiza wakulima kuongeza uzalishaji ili kuwe na tija ya kibiashara.
Katika Uzinduzi huo viongozi mbalimbali wameshiriki ambao ni pamoja na Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo; Mhe. Anthony Mavunde (Mb), Waziri wa Madini; Mhe. Innocent Bashungwa (Mb), Waziri wa Ujenzi; Mhe. Angela Kairuki (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii; Mhe. Jumaa Aweso (Mb), Waziri wa Maji, Mhe. Ummy Hamis Nderiananga (Mb), Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Viongozi Wakuu Watendaji wa Mkoa wa Katavi.
Wengine ni pamoja na Dkt. Andrew Komba, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Bw. Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji NIRC, Bodi Menejimenti na Watumishi wa NFRA; pamoja na wakulima na wananchi mbalimbali wa Mpanda.